Hamia kwenye habari

JANUARI 17, 2018
KAZAKHSTAN

Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa Imeisihi Kazakhstan Ichukue Hatua Kumsaidia Teymur Akhmedov

Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa Imeisihi Kazakhstan Ichukue Hatua Kumsaidia Teymur Akhmedov

Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imechukua hatua mara moja kufuatia malalamiko yaliyopelekwa Januari 3, 2018, yanayomhusu Teymur Akhmedov. Bw. Akhmedov mwenye umri wa miaka 61 na ambaye ni mgonjwa, amefungwa isivyo haki kwa karibu mwaka mmoja. Kwa kuwa mahakama za Kazakhstan zilikataa rufaa yake na zikaunga mkono hukumu aliyopewa kwa madai ya kushiriki utendaji wa kidini kinyume cha sheria, Bw. Akhmedov ametuma malalamiko yake kwenye Kamati hiyo ili apate msaada.

Katika ujumbe ulioandikwa Januari 9, 2018, Kamati iliisihi Kazakhstan ishughulikie hali ya afya ya Bw. Akhmedov hata kabla ya Kamati kutoa hukumu kuhusu malalamiko hayo. Iliwaeleza wenye mamlaka “wahakikishe kwamba [Bw. Akhmedov] anapata matibabu ya kutosha bila kukawia na kwamba mazingira ya kifungo chake yapatane kikamili na [Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa] na viwango vya kimataifa.” Isitoshe, mawasiliano hayo yaliwataka wenye mamlaka “wamwachilie kutoka gerezani kwa sababu ya matatizo ya afya anayokabili, au atolewe gerezani na kupewa kifungo cha nje wakati akisubiri Kamati ishughulikie malalamiko yake.”

Agizo ambalo serikali imepewa la kuhakikisha usalama wa Bw. Akhmedov linafanana na mapendekezo yaliyotolewa kumhusu na Kamati ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Vifungo Visivyo vya Haki. Mnamo Oktoba 2017, Kamati hiyo ilichunguza malalamiko ya Bw. Akhmedov na kugundua alihukumiwa isivyo haki na kwamba wenye mamlaka walipaswa kumwachilia mara moja na kumlipa fidia kwa kumtendea isivyo haki. Mpaka sasa, serikali ya Kazakhstan imepuuza utekelezaji wa mambo ambayo Kamati hiyo iliagiza. Bw. Akhmedov ametumikia mwaka mmoja hivi kati ya miaka mitano ya hukumu yake.