Hamia kwenye habari

FEBRUARI 22, 2018
KAZAKHSTAN

Maombi kwa Wenye Mamlaka wa Kazakhstan ya Kumwachilia Teymur Akhmedov

Maombi kwa Wenye Mamlaka wa Kazakhstan ya Kumwachilia Teymur Akhmedov

Familia na marafiki wa Teymur Akhmedov wanaendelea kuhangaishwa na hali yake. Bw. Akhmedov, Shahidi wa Yehova mwenye umri wa miaka 61, amekuwa akisumbuliwa na afya hata kabla ya kufungwa gerezani zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Februari 8, 2018, alifanyiwa upasuaji wa kuondoa sehemu mbili zenye uvimbe, lakini uvimbe mmoja ulioondolewa ulikuwa na kansa. Familia yake na mawakili wake wamewaomba wenye mamlaka wamwachilie kutoka kifungoni kwa sababu wanahangaishwa na hali katika gereza lililoko jijini Pavlodar na hali yake ya kiafya inayohitaji kushughulikiwa. Kufikia sasa maombi yao yamepuuzwa.

Mahakama nchini Kazakhstan zimemhukumu bila huruma Teymur Akhmedov kifungo cha miaka mitano gerezani, kifungo hicho kitakwisha mwaka wa 2022. Bw. Akhmedov hakufanya kosa lolote lakini alikamatwa na kuhukumiwa na wenye mamlaka kwa kutekeleza haki yake ya uhuru wa kuabudu. Wamemweka kwenye orodha ya majina ya watu waliofungiwa akaunti zao za benki kwa sababu wanashukiwa kuwa na mawasiliano na magaidi. Mahakama za Kazakhstan zimekataa rufaa zote alizoomba.

Kamati ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Vifungo Visivyo vya Haki imeipelekea serikali ya Kazakhstan mapendekezo yake, ikiwasihi wenye mamlaka wamwachilie Bw. Akhmedov na wafute mashtaka hayo ya uwongo yanayomkabili. Isitoshe, Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu imetoa agizo la haraka kwamba Kazakhstan imwachilie kutoka gerezani kwa sababu ya matatizo ya kiafya.

Wakili wa Bw. Akhmedov alisema hivi: “Kifungo kisicho cha haki cha Teymur, pamoja na matatizo ya kiafya na uhitaji wake wa kupata uangalifu wa kitiba, ni mambo yanayodai haki itendeke. Pamoja na maombi ya taasisi za Umoja wa Mataifa, sisi pia tunawaomba wenye mamlaka wa Kazakhstan wamwonyeshe huruma na kumwachilia Teymur kutoka gerezani bila kukawia.”