JUNI 28, 2017
KAZAKHSTAN
Mahakama ya Kazakhstan Yaunga Mkono Hukumu Isiyo ya Haki ya Teymur Akhmedov
Juni 20, 2017, Mahakama ya Jiji la Astana ilikataa rufaa ya Teymur Akhmedov kuhusu mashtaka ya uhalifu aliyoshtakiwa, iliunga mkono afungwe gerezani miaka mitano na ikamwongezea marufuku ya miaka mitatu ya kushiriki katika utendaji wake wa kidini. Mwanasheria wa kimataifa wa haki za kibinadamu aliyekuwepo mahakamani siku hiyo ya Juni 20 alisema hivi: “Huo ni ukiukaji wa sheria kwa sababu kulikuwa na uthibitisho wa kutosha wa kumuunga mkono Bw. Akhmedov.” Wakili wake wanafikiria kukata rufaa nyingine.
Mnamo Januari 2017, maofisa wa Kamati ya Usalama wa Taifa walimkamata na kumweka mahabusu Bw. Akhmedov kwa madai ya kufanya utendaji wa kidini kinyume cha sheria. Aliendelea kuwa mahabusu hadi kesi yake iliposikilizwa Mei 2, 2017. Siku hiyo Mahakama ya Wilaya ya Saryarkinskiy ilimhukumu isivyo haki kwa kutegemea kifungu cha 174 (2) cha Sheria ya Uhalifu ya Kazakhstan ambacho kinatoa adhabu kwa makosa ya uchochezi wa chuki ya kidini. Bw. Akhmedov alipinga kwa uthabiti madai hayo ya uwongo, akaeleza kwamba alikuwa tu akiwaeleza majirani wake imani yake ya dini na upendo wake kwao. Kutangaza imani ya dini ni haki ya msingi inayotolewa na Katiba ya Kazakhstan na mashirika ya kimataifa ya haki za kibinadamu ambayo Kazakhstan imekubali kufuata sheria zake.