Hamia kwenye habari

APRILI 18, 2018
KAZAKHSTAN

Teymur Akhmedov Ameachiliwa kwa Msamaha wa Rais

Teymur Akhmedov Ameachiliwa kwa Msamaha wa Rais

Aprili 2, 2018, Rais wa Kazakhstan Nursultan Nazarbayev alitoa msamaha kwa Teymur Akhmedov mwenye umri wa miaka 61, ambaye alikuwa amefungwa kwa zaidi ya mwaka mmoja kwa mashtaka ya uwongo. Msamaha huo umefuta rekodi yake ya uhalifu. Bw. Akhmedov alipata msamaha huo Aprili 4 na aliachiliwa kutoka kifungoni wakati akiwa hospitalini alikokuwa amefanyiwa upasuaji. Kwa sasa ameungana na familia yake na anaweza kupata kwa urahisi matibabu anayohitaji sana kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa kansa..

Kukamatwa, Kuwekwa Mahabusu, na Kufungwa Isivyo Haki

Bw. Akhmedov, ambaye ni Shahidi wa Yehova, alikamatwa na kufungwa Januari 18, 2017, kwa sababu tu ya kuwaeleza wengine kuhusu imani yake. Miezi kadhaa kabla ya kukamatwa, alikuwa akizungumzia habari za Biblia pamoja na wanaume fulani waliojifanya wanapendezwa sana na imani ya Mashahidi wa Yehova. Wanaume hao walikuwa wakishirikiana na polisi wa siri wa Kazakhstan, yaani, Kamati ya Usalama wa Taifa (KNB), na walikuwa wakirekodi kwa siri mazungumzo waliyokuwa wakifanya naye. Kwa kutegemea rekodi hizo, kamati hiyo ilimkamata Bw. Akhmedov na kumshtaki kwa “kuchochea chuki ya kidini” na kutangaza “kwamba dini [yake] ni bora” kulingana na Sheria ya Uhalifu ya 174(2) ya Kazakhstan.

Baada ya kumkamata, polisi walimhoji Bw. Akhmedov na kumweka mahabusu kwa miezi mitatu. Mei 2, 2017, mahakama ilimhukumu kifungo cha miaka mitano gerezani na ilimkataza asishiriki katika shughuli za dini kwa miaka mitatu baada ya kutoka gerezani.

Mawakili wa Bw. Akhmedov walikata rufaa nyingi ili aachiliwe, lakini mahakama zilikataa rufaa hizo zote. Alipokosa msaada wa kisheria nchini Kazakhstan, aliamua kupeleka malalamiko yake katika mashirika ya kimataifa ili asaidiwe. Alipeleka malalamiko kwenye Kamati ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Vifungo Visivyo vya Haki (WGAD) na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu.

Oktoba 2017, WGAD iliishutumu Kazakhstan kwa kumfunga Bw. Akhmedov na iliisihi serikali imwachilie haraka sana, kwa sababu kazi “aliyokuwa akifanya ilikuwa ya amani na hakuwa akikiuka uhuru wake wa kuabudu.” Mnamo Januari 2018, Kamati ya Haki za Kibinadamu ilikubali maombi ya haraka ya Bw. Akhmedov na iliagiza hatua ichukuliwe haraka sana, kwamba Kazakhstan ichukue hatua ya haraka kuhakikisha anapata matibabu yanayofaa. Kamati ya Haki za Kibinadamu ilisema kwamba Kazakhstan imwachilie Bw. Akhmedov wakati akiendelea kusubiri uamuzi wa malalamiko yake.

Hatimaye Aachiliwa

Teymur na Mafiza Akhmedov, baada ya kupata msamaha

Alipokuwa kifungoni, hali ya kiafya ya Bw. Akhmedov ilikuwa ikiendelea kuzorota. Mapema mwaka huu, madaktari walithibitisha kwamba alikuwa na kansa ya utumbo mpana na hali yake inaendelea kuwa mbaya sana. Kutokana na uamuzi wa Kamati ya Haki za Kibinadamu wa kuchukuliwa hatua haraka pamoja na maombi mengine mengi kutoka katika mashirika ya kimataifa, maofisa wa Kazakhstan walimweleza Bw. Akhmedov atume kwa Rais Nazarbayev maombi ya kuachiliwa.

Alituma maombi hayo Machi 5, 2018, na alieleza kwamba maombi yake yashughulikiwe haraka kwa sababu anahitaji matibabu ya haraka ili azuie kuenea kwa kansa. Wakati huohuo, maofisa wa gereza walimpeleka Bw. Akhmedov huko Almaty, Kazakhstan, ambako alifanyiwa upasuaji Machi 27, 2018.

Je, Kazakhstan Itaheshimu Zaidi Uhuru wa Ibada?

Bw. Akhmedov na mke wake, Mafiza, na watoto wao wanafurahi kwamba kipindi kigumu katika maisha yake kimepita. Pia, wanamshukuru Rais Nazarbayev kwa kumfutia rekodi zake zote za uhalifu. Kwa kuwa alihukumiwa kuwa mhalifu isivyo haki, serikali ilikuwa imefunga akaunti zake za benki alipokuwa gerezani, jambo lililofanya mke wake akabili hali ngumu sana.

Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wanatumaini kwamba kupewa msamaha kwa Bw. Akhmedov kunaonyesha kwamba maofisa wa serikali nchini Kazakhstan sasa watawapa Mashahidi uhuru zaidi wa kufanya ibada yao ya amani bila kuvurugwa.