Hamia kwenye habari

(Kushoto) Programu ya wakfu iliyofanyika katika ukumbi wa kukodisha. (Kulia) Majengo mawili mapya ya shule

NOVEMBA 20, 2019
KENYA

Majengo Mapya ya Shule ya Kitheokrasi Yawekwa Wakfu Nchini Kenya

Majengo Mapya ya Shule ya Kitheokrasi Yawekwa Wakfu Nchini Kenya

Novemba 9, 2019, majengo mapya ya shule ya Biblia yaliwekwa wakfu huko Eldoret, Kenya. Ndugu Bengt Olsson, mshiriki wa Halmashauri ya Tawi ya Kenya, alitoa hotuba ya wakfu mbele ya wahudhuriaji 1,199, kutia ndani watumishi 500 hivi wa pekee wa wakati wote waliosafiri kutoka sehemu mbalimbali za nchi. Majengo hayo ya shule yenye mita 433 za mraba yana madarasa kwa ajili ya Shule ya Waeneza-Injili wa Ufalme (SKE) na Shule ya Waangalizi wa Mzunguko na Wake Zao. Inatarajiwa kwamba angalau madarasa manne ya SKE yatahitimu kila mwaka katika majengo hayo.

Majengo hayo yanamilikiwa na ofisi ya tawi na zamani yalitumiwa kwa makusudi mengine. Jengo lililokuwa makao ya wamishonari lilirekebishwa kuwa dobi, eneo la jikoni, na chumba cha kulia chakula kwa ajili ya wanafunzi. Jumba la Ufalme lilibadilishwa kuwa darasa. Kazi hiyo ilianza Aprili 1, 2019, na kufikia Septemba 9 sehemu kubwa ilikuwa imekamilika.

Akizungumzia umuhimu wa shule hiyo, Ndugu Olsson alisema hivi: “Eneo la Afrika Mashariki lina uwezo mkubwa sana wa kupata ukuzi. Tuna uhakika kwamba mazoezi ambayo wanafunzi wa shule hizi watapata yatatimiza sehemu muhimu katika kushughulikia ongezeko kubwa wakati ujao kadiri watu wanavyomiminika kwenye mlima wa Yehova.”—Mika 4:1.