JULAI 5, 2023
KENYA
Uamuzi wa Mahakama Walinda Uhuru wa Ibada wa Wanafunzi wa Shule Nchini Kenya
Mei 12, 2023, Mahakama ya Rufaa ya Kenya ilitoa uamuzi muhimu unaotetea uhuru wa kidini wa wanafunzi wa shule nchini humo. Licha ya kwamba sheria ya Kenya inasema kwamba hakuna mtu anayepaswa kulazimishwa kushiriki katika utendaji wowote unaopingana na imani yake ya kidini, tangu mwaka wa 2015 wanafunzi 41 ambao ni watoto wa Mashahidi wa Yehova wamefukuzwa shule au kusimamishwa kwa muda kwa sababu ya kukataa kushiriki katika ibada ya dini nyingine.
Uamuzi huo wa Mahakama ya Rufaa unahusiana na jambo lililotokea mwaka wa 2017. Wanafunzi tisa walikataa kwa heshima kushiriki katika vipindi vya ibada ambavyo vingewalazimu kuchanganya imani wakiwa shuleni. Kesi yako ilipelekwa mahakamani. Mwaka wa 2019, mahakama ya chini ilitoa uamuzi wa kwamba shule hiyo haikukiuka haki za msingi za watoto Mashahidi kwa kuwalazimisha kushiriki vipindi hivyo. Hata hivyo, Mei 12, 2023, Mahakama ya Rufaa ya Kenya ilitangaza kwamba hilo “lilikiuka haki [ya mwanafunzi] ya kupata elimu na haki ya kutendewa kwa heshima.” Iliongezea pia kusema kwamba amri ya kuwataka Mashahidi wa Yehova kuhudhuria ibada ya dini nyingine ilikuwa “ya kibaguzi, isiyopatana na katiba, na batili.” Hakimu mmoja ambaye alishiriki katika kesi hiyo aliandika hivi: “Uamuzi wa Mahakama hii umekusudiwa kuwa mwongozo kwa shule zote kuhusiana na haki za kidini za wanafunzi.”
Uamuzi huu umeunga mkono agizo lililotolewa Machi 2022 na Wizara ya Elimu ya Kenya lililowaelekeza wakuu wa shule kuheshimu haki za kidini za wanafunzi wote. Pia, kwa sababu ya uamuzi huu, Kenya imeingia katika orodha inayoendelea kuongezeka ya nchi za Afrika ambazo zimetoa maamuzi yanayolinda haki za msingi za wanafunzi ambao ni Mashahidi, kama vile Malawi na Rwanda.
Vijana wetu jasiri nchini Kenya na ulimwenguni pote wanaweza kuwa na uhakika kwamba Yehova anajivunia kuwaona wakisimama imara kwa ajili ya ibada safi!—Methali 29:25.