Hamia kwenye habari

JANUARI 17, 2020
KOREA KUSINI

Korea Kusini Yatoa Msamaha wa Pekee kwa Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Korea Kusini Yatoa Msamaha wa Pekee kwa Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Desemba 31, 2019, serikali ya Korea Kusini ilitangaza kwamba watu 1,879 waliokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri na kuachiliwa huru, watapokea msamaha wa pekee. Ingawa bado ndugu hao watakuwa na rekodi ya uhalifu, serikali imefuta vizuizi walivyowekewa. Msamaha huo wa pekee umetokana na uamuzi wa mwaka 2018 uliofanywa na Mahakama ya Katiba pamoja na Mahakama Kuu uliotambua kwamba kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ni haki ya raia, na si tendo la uhalifu.

Serikali ya Korea Kusini huwawekea watu vizuizi vingine vinavyoendelea kwa miaka mitano baada ya vifungo vyao vya gerezani. Kwa kuwa watu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri wana rekodi ya uhalifu, serikali hiyo iliwawekea ndugu zetu vizuizi hivyo. Kwa sababu hiyo, akina ndugu walizuiwa kufanya mitihani ili kupata leseni zinazotambuliwa na taifa au kuomba kazi za aina fulani.

Ndugu Hong Dae-il, anayeratibu kazi katika Dawati la Habari za Umma nchini Korea Kusini, anasema hivi: “Tunashukuru serikali kwa kuondoa vizuizi hivyo. Hii ni hatua nzuri itakayosaidia watu watambue kikamili kwamba wale waliofungwa kwa sababu ya dhamiri hawapaswi kuonwa kuwa wahalifu.”

Tunapoendelea kutazamia maendeleo mazuri nchini Korea Kusini, tunampa Yehova utukufu na heshima, Mpaji-Sheria mkuu zaidi.—Ufunuo 4:11.