Hamia kwenye habari

Mahakama yatoa uamuzi unaounga mkono msimamo wa Ndugu Nam Eon-woo (kushoto), Lee Jeong-Hyeon (katikati), na Nam Tae-hee (kulia), waliotumikia jeshi kabla ya kuwa Mashahidi wa Yehova na baadaye wakashtakiwa na kuendelea kuadhibiwa kisheria

MACHI 3, 2021
KOREA KUSINI

Mahakama Kuu ya Korea Yaunga Mkono Waliokataa Kutumikia Jeshi la Akiba kwa Sababu ya Dhamiri

Mahakama Kuu ya Korea Yaunga Mkono Waliokataa Kutumikia Jeshi la Akiba kwa Sababu ya Dhamiri

Januari 28, 2021, Mahakama Kuu ya Korea Kusini ilifika uamuzi wa kwamba si kosa ikiwa mtu atakataa kujiunga na jeshi la akiba kwa sababu ya dhamiri. Sasa, ndugu zetu waliotumikia jeshi kabla ya kuwa Mashahidi wa Yehova hawataendelea kuadhibiwa kisheria.

Kila baada ya kipindi fulani cha wakati, wanaume wote waliotumikia jeshi la Korea Kusini wanapaswa kupata mafunzo ya jeshi la akiba kwa miaka nane. Hilo lilimaanisha kwamba ndugu zetu ambao zamani walikuwa wanajeshi, wangeitwa na kuadhibiwa mara kadhaa kwa kukataa mafunzo hayo. Ndugu mmoja alihitaji kwenda polisi, katika ofisi ya mwendesha-mashtaka, na mahakama zilizoshughulikia kesi na rufaa zaidi ya mara 60 hivi, ndani ya mwaka mmoja.

Katika mwaka wa 2018, mahakama kuu mbili za Korea, Mahakama ya Katiba na Mahakama Kuu, zilitoa uamuzi wa kwamba kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri si kosa na uamuzi huo ulikuwa msingi wa kuanzishwa kwa utumishi wa badala wa kiraia. Hata hivyo, Mahakama hizo hazikuzungumzia Sheria ya Jeshi la Akiba inayosema kwamba, adhabu inaweza kutolewa kwa wale wote wanaokataa mafunzo ili kuwa askari wa akiba kwa sababu ya imani yao.

Hatimaye uamuzi wa hivi karibuni wa Mahakama Kuu unatambua kwamba ni jambo la kisheria kukataa mafunzo ya kuwa askari wa akiba. Akina ndugu ambao wamevumilia kwa muda mrefu kesi dhidi yao, sasa wanaweza kuomba kufanya utumishi wa badala wa kiraia badala ya kutozwa faini na kufungwa gerezani. Ndugu Nam Tae-hee, mmoja wa washtakiwa katika kesi hiyo alisema hivi: “Baada ya kwenda mahakamani mara nyingi katika kipindi cha miaka nane, hatimaye sasa haki zangu zinatambuliwa. Ninahisi kana kwamba nimetua mzigo mzito.”

Tunafurahi na kumshukuru Yehova pamoja na ndugu zetu wa Korea na familia zao kwa ‘kuvumilia taabu na kuteseka isivyo haki kwa sababu ya dhamiri kwa Mungu’!—1 Petro 2:19.