Hamia kwenye habari

DESEMBA 12, 2019
KOREA KUSINI

Mateso ya Mashahidi Nchini Korea Yafunuliwa Katika Jumba la Makumbusho ya Taifa

Mateso ya Mashahidi Nchini Korea Yafunuliwa Katika Jumba la Makumbusho ya Taifa

Sehemu ya historia ya Mashahidi wa Yehova ambayo haijulikani sana iliwekwa katika Jumba la Makumbusho la Taifa la Utumishi wa Kulazimishwa Chini ya Ukoloni wa Japani, katika jiji la pili kwa ukubwa nchini Korea, Busan. Maonyesho hayo ya pekee yenye kichwa “Historia Inayobadilika, Dhamiri Isiyobadilika” yalianza Novemba 12, 2019, na kumalizika Desemba 13, 2019. Yalionyesha msimamo wa kutojihusisha na siasa wa Mashahidi zaidi ya miaka 80 iliyopita nchini Korea, chini ya ukoloni wa Japani na mateso yaliyowapata.

Maonyesho hayo yalifanyika kwa mara ya kwanza Septemba 2019 kwenye ukumbi wa Seodaemun Prison History a ulio jijini Seoul. Yaliwavutia wageni 51,175, kutia ndani ndugu na dada 5,700 ambao waliokuwa wajumbe katika kusanyiko la kimataifa huko Seoul.

Tukio la Deungdaesa lilifanyika wakati Mashahidi wa Yehova na wale waliopendezwa na ujumbe wa Biblia walipokamatwa na kufungwa kuanzia Juni 1939 hadi Agosti 1945. Watu hao walifungwa kwa kukataa kujihusisha na ibada ya maliki na kwa madai ya kueneza propaganda za kupinga vita. Watu sitini na sita walikamatwa, ambayo ni idadi sawa na Mashahidi wa Yehova wote waliokuwa nchini Korea wakati huo. Wale waliofungwa waliteswa kikatili. Mashahidi sita walikufa kutokana na hali mbaya zilizokuwa gerezani.

Ndugu Hong Dae-il, mratibu wa Dawati la Habari za Umma nchini Korea, alisema hivi: “Watu wengi nchini Korea hawajui kwamba suala la haki za kibinadamu kuhusu kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri lilianza miaka 80 iliyopita chini ya utawala wa Wajapani. Maonyesho haya ya pekee, yametokeza fursa nzuri ya kuwaeleza watu kwa mara ya kwanza kuhusu mambo yaliyotokea.”

Profesa Han Hong-gu, mwanahistoria aliyetembelea maonyesho hayo siku ya kwanza alisema hivi kuhusu wale waliosimama imara kwa ajili ya imani yao: “Ninaamini kwamba wameweka mfano bora zaidi inapohusu masuala ya dhamiri. . . . Jamii yetu inapozidi kuelewa umuhimu wa kuheshimu watu wanaotii dhamiri zao, watu hao wanapaswa kuwa wa kwanza kukumbukwa.”

Maonyesho haya yamepata itikio zuri kutoka kwa wanahistoria na waandishi wa habari, na kutokeza fursa nzuri ya kujulisha watu kuhusu historia ya watu waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri—suala ambalo limezungumziwa sana nchini Korea mwaka uliopita. Juni 28, 2018, Mahakama ya Katiba ilisema kwamba kulingana na katiba utumishi wa badala ni jambo linalopaswa kuwepo. Kisha baada ya miezi minne tu, Novemba 1, Mahakama Kuu iliamua kwamba kukataa utumishi wa kijeshi si kosa la uhalifu. Baada ya uamuzi huo wa mahakama ndugu zetu waliokuwa wamefungwa kwa kosa la kukataa utumishi wa kijeshi Korea Kusini waliachiliwa na pia hilo likaweka msingi wa kutunga sheria ya utumishi wa badala wa kiraia.

Imani yenye nguvu na ujasiri thabiti wa ndugu na dada zetu wa zamani nchini Korea unatukumbusha maneno haya: “Yehova yuko upande wangu; sitaogopa. Mwanadamu atanifanya nini?”—Zaburi 118:6.

a Kabla ya maonyesho ya History Hall kuanzishwa, gereza hili lilitumiwa kuwafunga wale waliokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri kuanzia miaka ya 1960 hadi 1980, na pia Mashahidi wa Yehova wakati wa utawala wa Wajapani.

 

Makumbusho ya History Hall katika gereza la Seodaemun huko huko Seoul, Korea. Maonyesho hayo yalifanyika hapa kwa mara ya kwanza Septemba 2019

Kikundi cha wanafunzi nje ya Ukumbi wa maonyesho ya History Hallhuko Deungdaesa, jumla ya watu 51,175 walitembelea sehemu hiyo

Katika eneo hili kuna mfano wa mnara wa mlinzi ambao ulitumiwa katika gereza hili

Chumba cha gereza chenye mifano ya wafungwa watano kinachoonyesha hali ambayo Mashahidi walikabili gerezani

Maonyesho hayo yako kwenye Makumbusho ya Kitaifa ya Busan yaUtumishi wa Kulazimishwa Chini ya Utawala wa Japani

Sehemu ya mwisho ya makumbusho hayo ni ukuta waenye michoro kuhusu hadithi za watu 66 walioteswa kwa sababu ya kutounga mkono masuala ya kisiasa