Hamia kwenye habari

MEI 9, 2016
KOREA KUSINI

Je, Korea Kusini Italinda Uhuru wa Dhamiri?

Je, Korea Kusini Italinda Uhuru wa Dhamiri?

Seon-hyeok Kim anakabili changamoto kubwa katika maisha yake. Mwanzoni mwa mwaka wa 2015, mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 28 ambaye ni mume na baba alipelekwa mahakamani akishtakiwa kosa la jinai la kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu dhamiri. Kwa kuwa Mahakama ya Wilaya ya Gwangju ilifuata viwango vya kimataifa ilimtangaza kwamba hana hatia. Uamuzi huo ulikuwa wa pekee nchini Korea Kusini, ambapo kwa miaka mingi maelfu ya watu waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri wametiwa hatiani na kufungwa. Hata hivyo, mahakama ya rufani ilibadili uamuzi wa kesi ya Bw. Kim na kumhukumu kifungo cha miezi 18 gerezani. Rufani aliyokata bado haijasikilizwa na Mahakama ya Juu Zaidi ya Korea Kusini.

Katika miaka ya karibuni kumekuwa na hali ya kutokubaliana nchini Korea Kusini kuhusiana na suala la kukataa kuwatambua wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Uamuzi wa mahakimu wanaoamua kwa ujasiri kuunga mkono viwango vya kimataifa kuhusiana na suala hili, unapingwa wakati wa rufani.

Mahakama ya Wilaya Yatetea Haki ya Uhuru wa Dhamiri

Mei 12, 2015, Hakimu Chang-seok Choi wa Mahakama ya Wilaya ya Gwangju alimwachilia huru Bw. Kim aliyeshtakiwa kosa la kukataa kujiunga na jeshi, na alieleza kwamba Bw. Kim hakuwa akipuuza wajibu kwa taifa. Badala yake, alisema kwamba Bw. Kim, ni Shahidi wa Yehova mwenye imani thabiti na dhamiri yake haimruhusu kutumikia jeshini. Hakimu alisema Bw. Kim alikuwa tayari kufanya utumishi wa badala wa umma ambao hauhusishi utumishi wa jeshi. a

Alipokuwa akitoa hukumu, Hakimu Choi aliendelea kueleza kwamba Bw. Kim alikuwa akitumia haki yake ya uhuru wa dhamiri alipokataa kujiunga na jeshi na kwamba “uhuru wa dhamiri unapaswa kulindwa.” Kwa ujasiri, Hakimu Choi alionyesha anaheshimu uhuru wa dhamiri wa Bw. Kim. Uamuzi wa hakimu huyo ulikuwa tofauti na maamuzi mengine ya kesi za aina hiyo nchini humo lakini ulipatana na viwango vya kimataifa vilivyowekwa kuhusiana na wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

“Uhuru wa dhamiri unapaswa kulindwa, jambo linaloweza kufanywa kwa njia rahisi bila kupingana na wajibu wa msingi wa kulinda taifa.”—Jaji Chang-seok Choi, Mahakama ya Wilaya ya Gwangju

Katika maamuzi matano tofauti ya malalamishi zaidi ya 500, Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu (CCPR) imeilaumu nchi ya Korea Kusini kwa kuwaadhibu watu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Uamuzi uliotolewa hivi karibuni na CCPR ulieleza kwamba kuwafunga watu hao ni sawa na kuwaweka watu kizuizini kinyume na sheria kwa mujibu wa Kipengele cha 9 cha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR). b CCPR na mashirika mengine ya kimataifa yameisihi Korea Kusini ipitishe sheria inayoruhusu utumishi wa badala wa kiraia kwa ajili ya wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Ingawa Korea Kusini ilijiunga kwa hiari na ICCPR mwaka wa 1990 na pia katika Mkataba wake wa Kwanza wa Ziada, imekataa kuchukua hatua zaidi za kutekeleza maamuzi hayo.

Ni Mwenye Hatia au La?

Mwendesha-mashtaka alikata rufani ili kupinga uamuzi wa kuachiliwa huru kwa Bw. Kim, akidai kwamba kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kunatishia usalama wa taifa. c Novemba 26, 2015, mahakama ya rufani ilibadili uamuzi wa awali wa mahakama uliomhukumu Bw. Kim kuwa hana hatia na kumhukumu kifungo cha miezi 18 gerezani kwa kukataa kujiunga na jeshi.

Ingawa mahakama ya rufani ilitambua maoni ya CCPR, ilijitetea kwa kudai kwamba katika kesi hiyo mahakama za Korea Kusini zina mamlaka zaidi kuliko sheria ya kimataifa. Mara moja Bw. Kim alikata rufani katika Mahakama ya Juu Zaidi na akatuma malalamiko yake kwenye Kikundi cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulikia Vifungo Visivyozingatia Misingi ya Kisheria. d Anasubiri maamuzi kutoka katika sehemu hizo mbili.

Mahakama ya Juu zaidi na Mahakama ya Katiba zimeendelea kukataa kutambua haki ya watu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Katika mwaka wa 2004 na tena katika mwaka wa 2011, Mahakama ya Katiba iliiona Sheria ya Utumishi wa Jeshi kuwa haipingani na katiba ya nchi. Sasa Mahakama ya Katiba inachunguza kwa mara ya tatu uhalali wa Sheria ya Utumishi wa Jeshi na inatarajia kutoa uamuzi wake hivi karibuni.

Tangu mwaka wa 1953, mahakama za Korea Kusini zimewafunga gerezani zaidi ya Mashahidi 18,000 wa Yehova kwa sababu ya kukataa kujiunga na jeshi.

Je, Korea Kusini Hatimaye Itatambua Viwango vya Kimataifa?

Ikiwa Mahakama ya Juu Zaidi itakataa rufani ya Bw. Kim, atafungwa gerezani. Ana wasiwasi kujua kwamba kwa miezi 18 atakayokuwa gerezani familia yake itaathirika kihisia na kiuchumi. Mke wake ndiye atakayewaandalia na kuwatunza watoto wao wawili bila msaada. Baada ya kutoka gerezani, itakuwa vigumu kwake kuajiriwa kwa sababu ya kuwa na rekodi ya uhalifu.

Mashahidi wa Yehova wanafurahi kwamba serikali mbalimbali duniani pote zimekubali kiwango cha kimataifa cha kutambua haki ya watu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Seon-hyeok Kim pamoja na Mashahidi wote wa Yehova nchini Korea Kusini wanatarajia mahakama zitatue tatizo hili. Je, Mahakama ya Juu Zaidi na Mahakama ya Katiba zitafuata viwango vya kimataifa walivyovikubali kwa hiari? Je, Korea Kusini itaheshimu uamuzi wa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kama haki ya msingi ya raia wake?

a Mwaka 2015, Mahakama ya Wilaya ya Gwangju iliwahukumu Mashahidi wengine watatu kuwa “hawana hatia.” Pia Mahakama ya Wilaya ya Suwon iliwaachilia huru Mashahidi wawili katika kesi ya kukataa kujiunga na jeshi.

b Kamati ya Haki za Kibinadamu, Maoni, Young-kwan Kim et al. v. Republic of Korea, Ujumbe Na. 2179/2012, U.N. Doc. CCPR/C/112/D/2179/2012, Oktoba 15, 2014

c Mwendesha-mashtaka alilalamika kwamba wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri watakuwa na uvutano mbaya kuelekea usalama wa taifa. Hata hivyo, wanasheria wengine hawakubaliani na maoni yake. Kwa mfano, Hakimu Gwan-gu Kim wa Mahakama ya Wilaya ya Changwon Masan alisema hivi, “Hakuna uthibitisho wa msingi, hususa, au habari zozote zinazopatikana zinazothibitisha kwamba kukubali mfumo wa utumishi wa badala kutadhoofisha usalama wa taifa.”

d WGAD inaandaa mfumo wa kukata rufani kwa kuingilia na kuzuia kifungo ikiwa sababu ya kifungo hicho kinahusiana na haki za msingi au uhuru unaotolewa na sheria ya kimataifa ya haki za kibinadamu.