Hamia kwenye habari

NOVEMBA 27, 2015
KOREA KUSINI

Mashahidi Zaidi ya 600 Nchini Korea Wapeleka Malalamiko Kwenye Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Vifungo Visivyo vya Haki

Mashahidi Zaidi ya 600 Nchini Korea Wapeleka Malalamiko Kwenye Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Vifungo Visivyo vya Haki

Vijana zaidi ya 600 waliofungwa jela nchini Korea Kusini waliwasilisha malalamiko yao mwezi wa Julai na Agosti 2015 kwenye Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Vifungo Visivyo vya Haki. Kila mmoja wao alikuwa amekamatwa kwa kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya imani yake ya dini, akashtakiwa kama mhalifu, na kuhukumiwa kifungo cha miezi 18 gerezani.

Sababu ya Kuwasilisha Malalamiko

Oktoba 15, 2014, Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu ilitoa uamuzi kwamba Korea Kusini ilikuwa na hatia ya kuwafunga watu bila misingi ya kisheria ilipowafunga gerezani wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Uamuzi huo umekuwa msingi wa malalamishi ya wafungwa hao yaliyopelekwa kwenye Kamati hiyo.

Jukumu la Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Vifungo Visivyo vya Haki ni “kuchunguza visa vya kuwanyima watu uhuru vinavyotekelezwa kinyume cha sheria au visivyopatana na . . . sheria za kimataifa zilizokubaliwa na Serikali zinazohusika.”

Du-jin Oh, wakili wa walalamishi, anaeleza kwa nini hakuna msingi wa kisheria wa kuwafunga wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Kulingana na kiwango cha kimataifa serikali inapaswa kuandaa utumishi wa badala unaokubalika kwa ajili ya raia wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri inaambatana na haki ya uhuru wa dhamiri na wa kidini. Hata hivyo, serikali ya Korea Kusini inaendelea kupuuza wito wa jamii ya kimataifa unaoitaka serikali hiyo iandae utumishi wa badala wa kiraia.

Mtu asiyeunga mkono upande wowote angesema kwamba uamuzi wa Korea Kusini wa kukataa kutatua tatizo ambalo limeendelea kwa miaka 60 na ambalo limeathiri maisha ya watu zaidi ya 18,000 pamoja na familia zao “hauna msingi wa kisheria.” Serikali imeshindwa kuandaa “suluhisho linalofaa” kwa ajili ya wanaume hao ili kutii maamuzi matano tofauti yaliyotolewa na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu. Kwa hakika si haki na ni ukandamizaji kuwafunga kama wahalifu watu walioazimia kutomdhuru mtu yeyote.

Malalamiko Yaliyowasilishwa Kwenye Kamati Hiyo

Wanaume hao wa Korea Kusini walipeleka malalamiko kwenye Kamati hiyo na kuiomba itende kwa niaba yao ili:

  • “Kuamua kwamba kifungo cha walalamikaji hao kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri hakina msingi wa kisheria.”

  • “Kuiagiza Jamhuri ya Korea iwaachilie huru mara moja walalamikaji hao na kufuta rekodi kwamba wao ni wahalifu.”

Alifungwa Gerezani kwa Sababu ya Imani Yake

Mfungwa mmoja anaitwa Jun-hyeok An. Kama wengine, yeye hajioni kuwa mhalifu. Mama yake alimfundisha kutumia kanuni za Biblia tangu alipokuwa mtoto. Alipokuwa kijana mdogo, aliamua kwamba kujiunga na jeshi hakupatani na imani yake ya kidini wala na dhamiri yake. a Alitafakari sana kabla ya kufanya uamuzi, akijua jinsi hali ilivyo Korea Kusini na akitambua matokeo ya kukataa kujiunga na jeshi. Alisema hivi:

Siamini kwamba ninapaswa kupata adhabu ya kufungwa kwa sababu ya kushikamana na imani yangu ya dini. Ikiwa serikali ingeandaa utumishi wa badala wa kiraia, ningeufanya. Uamuzi wangu unaotegemea imani wa kutomdhuru mtu yeyote haupaswi kunifanya nifungwe kama mhalifu na kuadhibiwa.

Korea Kusini Itaitikiaje Mwito Unaodai Ibadili Msimamo?

Kamati hiyo itapeleka orodha ya malalamiko 631 kwenye serikali ya Korea Kusini ili kupata maelezo yake. Serikali itakapotoa maelezo, Kamati hiyo itaeleza maoni yake na kutoa mapendekezo kwa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Kibinadamu. Ikiwa baraza hilo litakubali kwamba kufungwa kwa waliokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri hakukuwa na msingi wa kisheria, serikali ya Korea itawekewa vizuizi kwa kukiuka haki za kibinadamu licha ya kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Bw. Oh alisema hivi pia:

Kufikia sasa, Korea Kusini imekataa wito wa mataifa mengine wa kuitaka serikali yake iandae sheria inayoruhusu utumishi wa badala wa kiraia kwa ajili ya wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Wakati huohuo, maamuzi yanayofanywa na mahakama nchini humo yanazidi kuishinikiza serikali. Katika miezi ya karibuni, mahakimu wawili wa mahakama za wilaya wametoa uamuzi kwamba washtakiwa sita hawana hatia kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Tangu 2012, mahakimu wamepeleka kesi saba kwenye Mahakama ya Jimbo. Mahakama hiyo ilianza kusikiliza kesi hizo mnamo Julai 2015.

Kwa sasa, serikali ya Korea Kusini inawahukumu na kuwafunga gerezani Mashahidi 40 hadi 50 kila mwezi, na hivyo kukiuka sheria ya kimataifa. Bw. An na Mashahidi wote waliofungwa kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri nchini Korea Kusini wanasubiri kwa hamu uamuzi wa Mahakama ya Jimbo na wa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa.