SEPTEMBA 8, 2017
KOREA KUSINI
Watu Wengi Watoa Maoni Kuhusu Kutambuliwa kwa Haki ya Kukataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri Nchini Korea Kusini
Watu wengi nchini Korea Kusini wanafurahia mkataa uliofikiwa katika mkutano wa jamii wa Julai 2015 uliohusu Mahakama ya Kikatiba ya nchi hiyo. Hata ingawa hakuna uamuzi uliofanywa na mahakama au sheria mpya iliyotungwa, Korea Kusini imeboresha maoni yake kuhusu wale wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Maoni ya mahakama za chini, jamii, taasisi za kisheria, na taasisi za kitaifa na kimataifa za haki za kibinadamu zinakubaliana kwamba suluhisho litakalotolewa lisiwe adhabu kwa sababu ya kuongozwa na uhuru wa dhamiri.
Mabadiliko Yasiyotarajiwa ya Maoni ya Mahakama
Katika juma la Agosti 7, 2017, mahakama iliamua kwamba vijana saba walioshtakiwa kwa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri hawana hatia. Hakujawahi kuwa na uamuzi kama huo kabla ya hapo. Historia ya kisheria ya Jamhuri ya Korea inaonyesha kwamba mahakama zimewahukumu watu zaidi ya 19,000 waliokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri, lakini tangu Mei 2015, wahusika katika kesi 38 kati ya 39 waliambiwa na mahakama hawana hatia, na 25 kati ya kesi hizo zimesikilizwa mwaka wa 2017.
Baadhi ya mahakama zimeahirisha kesi hizo zikitumaini kupata uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba, na hilo limesababisha kuongezeka kwa kesi zinazosubiri kusikilizwa zinazohusu kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Bw. Du-jin Oh, wakili ambaye amewakilisha wengi wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, ameeleza kwamba kwa sasa kesi kuhusu jambo hili zinazosubiri kusikilizwa ni mara tano zaidi ya ilivyokuwa miaka michache iliyopita.
Watu waliotolewa uamuzi wa kutokuwa na hatia wameongezeka (6 mwaka 2015, 7 mwaka 2016, na 25 mwaka 2017) na kesi zilizoahirishwa zimeongezeka pia (kawaida ziliahirishwa kesi 100 hivi lakini sasa kesi 500 hivi). Hilo linaonyesha mabadiliko ya maoni ya mahakama nchini Korea Kusini.
Watu wengi wameona kwamba fikira za mahakama za Korea Kusini zimebadilika. Mahakama zinapotoa uamuzi wa kutokuwa na hatia zinatambua kwamba kuwaadhibu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri wakati hakuna utumishi wa badala wa kiraia ni ukiukwaji wa sheria zilizopo kwenye katiba zinazowapa raia uhuru wa dhamiri. Wengine wametambua kwamba kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi ni “sababu ya msingi” ya kukataa kujiandikisha jeshini kama Sheria ya Utumishi wa Kijeshi inavyosema.
Maoni ya Jamii
Ingawa maoni ya jamii si kigezo cha kutambua na kulinda haki za kibinadamu, Wizara ya Ulinzi imekuwa ikikataa kusuluhisha tatizo hilo kwa sababu linaungwa mkono na watu wachache. Lakini maoni ya watu wengi yanabadilika. Utafiti uliofanywa mwaka wa 2005, ulionyesha kwamba ni asilimia 10 tu ya watu waliokubali wazo la kutambua haki za wale wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Hata hivyo, ripoti ya uchunguzi uliofanywa Mei 2016 ilisema kwamba asilimia 70 ya walioshiriki waliunga mkono kuchukuliwa kwa hatua za ziada ili programu ya utumishi wa badala wa kiraia itekelezwe. Na uchunguzi uliofanywa Julai 2016 na Shirika la Seoul Bar (Seoul Bar Association) ulionyesha kwamba asilimia 80 ya watu waliunga mkono kuanzishwa kwa utumishi wa badala wa kiraia.
Maoni na Maamuzi ya Taasisi za Haki za Binadamu
Tume ya Haki za Kibinadamu ya Korea (NHRC) imetambua kwamba mabadiliko ya maoni ya watu nchini Korea Kusini yamekuwa yakiwachochea wabunge waunge mkono kuanzishwa kwa utumishi wa badala wa kiraia miswada mitatu tofauti ilipojadiliwa bungeni katika vipindi vya bunge vilivyoanza Juni 2017. Tume hiyo pia imekazia uangalifu maoni na maamuzi ya taasisi za kimataifa zinazosihi kutekelezwa kwa hatua hii na kisha kuchunguza jinsi mswada huo unavyokidhi viwango vya kimataifa vya utumishi wa badala wa kiraia. Tume pia imeipatia serikali ya Korea Kusini maoni yake kuhusu programu ya utumishi wa badala wa kiraia ambayo inakidhi viwango vya kimataifa na ambayo imekuwa ikikubaliwa na Mashahidi wa Yehova na watu wengine.
Ahadi na Ombi
Rais Jae-in Moon alipoanza kazi rasmi Mei 10, 2017, aliingia kwenye ofisi hiyo akiwa na uzoefu kwa kuwa yeye ni mwanasheria wa haki za binadamu na aliahidi hivi: “Uhuru wa dhamiri ni haki ya msingi kuliko haki zote za msingi zilizo kwenye Katiba. Kwa hiyo, ninaahidi kuanzisha utumishi wa badala wa kiraia na kuondoa mazoea yaliyopo ya kuwafunga wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.”
Agosti 11, 2017, wajumbe waliowakilisha watu 904 waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri waliwasilisha ombi lao kwa rais mpya, wakiomba serikali itambue haki za wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kwa kuwaachilia kutoka katika vifungo vyao na kuwapatia utumishi wa badala wa kiraia. Pia, watu hao walitoa ombi hilo kwa ajili ya watu 360 ambao wanatumikia vifungo vyao na wengine 544 ambao kesi zao zipo katika mahakama mbalimbali nchini.
Nafasi ya Kufanya Uamuzi wa Kihistoria wa Haki za Kibinadamu
Hyun-soo Kim, mmoja wa watu waliotoa ombi hilo, alifafanua jinsi ambavyo ombi hilo lingeathiri maisha yake kwa kusema hivi: “Ninatarajia kuanzishwa kwa utumishi wa badala wa kiraia ambao unakidhi viwango vya kimataifa, ambao utakuwa utumishi wa kiraia kikamili usiohusiana hata kidogo wala kusimamiwa na jeshi. Nipo tayari kutumikia katika eneo litakalonufaisha jamii au kusaidia wakati wa majanga au eneo lolote ambalo nitapangiwa. Nitafurahia sana kusaidia jamii.”
Mashahidi wa Yehova na watu wengine wanafurahi sana kuona mabadiliko hayo ya maoni ya watu ambayo yanaweza kusaidia kubadili sera ambayo imefanya maelfu ya wanaume kuadhibiwa kwa miaka 70 hivi. Mashahidi wanafurahi sana kwamba rais Moon, washiriki wa Bunge, na mahakama za Korea Kusini wameonyesha kuwa tayari kuheshimu na kutimiza mahitaji ya wale wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu dhamiri.