DESEMBA 20, 2016
KOREA KUSINI
Mahakama ya Kikatiba ya Korea Kusini Itatoa Uamuzi Muhimu Hivi Karibuni
Mahakama ya Kikatiba ya Korea Kusini inasubiriwa ifanye uamuzi wa kihistoria kwa kuwa imepewa daraka la kuchunguza kwa mara nyingine ikiwa kanuni za katiba zinapatana na adhabu inayotolewa kwa wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri chini ya Sheria za Utumishi wa Kijeshi. Mahakama hiyo imekuwa ikitarajiwa itoe uamuzi huo tangu Julai 2015 wakati uchunguzi wa suala hilo ulipoanza kufanywa. Karibuni, Rais wa Mahakama hiyo, Han-chul Park, alithibitisha kwamba uamuzi huo utatolewa mapema kabla ya kumalizika kwa kipindi cha uongozi wake, yaani, Januari 30, 2017.
Matokeo Yatakayonufaisha Maelfu ya Watu
Mahakama ya Kikatiba ya Korea Kusini ndiyo mahakama kubwa zaidi nchini humo iliyo na mamlaka ya kuamua ikiwa sheria inapatana na katiba. Mahakama hiyo imeombwa ichunguze upya sehemu iliyo katika Sheria ya Utumishi wa Kijeshi inayowaadhibu watu kwa kuwafunga wanapokataa kujiunga na jeshi kwa sababu dhamiri. Mahakama hiyo inatarajiwa iamue ikiwa adhabu hiyo inapingana na Katiba ya Korea Kusini pamoja na haki ya uhuru wa dhamiri na dini.
Ikiwa Mahakama hiyo itaamua kwamba zoea la muda mrefu la serikali kuwafunga wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri halipatani na katiba, Korea Kusini italazimika kuchunguza upya jinsi inavyowatendea watu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Inawezekana matokeo hayo mazuri yakafanya serikali iache kuwafungulia mashtaka, kuwahukumu, na kuwafunga vijana wanaokataa kufanya utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.
Mvurugo Katika Utaratibu wa Mahakama
Mahakama ya Katiba ilichunguza jambo hilo katika mwaka wa 2004 na 2011. Mara zote mbili, mahakama ilitoa uamuzi kwamba sheria za kuwahukumu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zinapatana na katiba. Vivyo hivyo, Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa ya Korea Kusini, na mahakama iliyoshughulikia kesi hii kwa mara ya mwisho zilitoa uamuzi katika mwaka wa 2004 na 2007 kwamba kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri si sababu ya msingi ya kukataa kujiandikisha jeshini. Licha ya maamuzi hayo katika mahakama za juu, utekelezwaji wa sheria ni tatizo la muda mrefu hata mahakamani.
Mahakama za Korea Kusini katika kila ngazi zimeonyeshwa kutoridhishwa na hukumu ya vifungo vya gerezani vinavyotolewa kwa wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Tangu Mahakama ya Kikatiba itoe uamuzi wake kuhusiana na suala hili mwaka wa 2011, imekubali kusikiliza kesi 7 za rufaa kutoka kwa mahakama za wilaya na nyingine 22 zilizoletwa na watu. Pia, maamuzi yaliyofanywa na Mahakama Kuu yamepingwa, na kuna zaidi ya kesi 40 za watu waliokataa kujiunga na jeshi wa sababu ya dhamiri zinazosubiri uamuzi wa mahakama hiyo kuu. Tangu Mei 2015, mahakama mbalimbali zimeamua kesi tisa kuwa wahusika hawakuwa na hatia kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.
Oktoba 2016, mahakama ya rufaa ilitambua changamoto zinazokabili mahakama za chini na za juu, ikaeleza hivi: “Kuna mvurugo mwingi sana kuhusu ufafanuzi na matumizi ya sheria hii moja.” Katika maamuzi yake ya mwanzoni, mahakama hiyo ya rufani ilitangaza kuwaondolea hatia watu watatu waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Uamuzi huo wa kuwaondolea hatia ulipokewa vizuri na Shirika la Seoul Bar (Seoul Bar Association), ambalo lilisema uamuzi huo ni wa “kihistoria.” Rais wa shirika hilo, Han-kyu Kim, alisema kwamba sasa, Mahakama ya Kikatiba ndiyo itakayotoa uamuzi wa mwisho.
“Kuna mvurugo mwingi sana kuhusu ufafanuzi na matumizi ya sheria hii moja.”—Mahakama ya Wilaya ya Gwangju, Kta ya Tatu ya Uhalifu, uamuzi wa hukumu katika kesi ya Lak-hoon Cho, iliyofanywa Oktoba 18, 2016
Suala la Muda Mrefu Linalokaribia Kutatuliwa
Bw. Kim aliongezea kusema hivi: “Wananchi wanasubiri kwa hamu uamuzi mzuri [wa Mahakama ya Kikatiba] kuhusiana na suala hili. Wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri bado wanaendelea kuadhibiwa kama wahalifu hata bila kupewa nafasi ya kufanya utumishi wa badala wa kiraia. Mahakama ya Kikatiba, ambayo ndiyo mahakama ya juu zaidi yenye nguvu za kutetea haki za kibinadamu, imeombwa itoe uamuzi wake haraka iwezekanavyo.”
Kwa zaidi ya miaka 60 sasa, karibu kila familia ya Mashahidi wa Yehova nchini Korea Kusini imeguswa na suala hili, kwa sababu iwe ni baba, wana, au ndugu wamefungwa gerezani kwa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Uamuzi utakaowaunga mkono wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri utaondoa vifungo visivyozingatia haki na rekodi mbaya za uhalifu ambazo vijana wengi wanapata na kutaimarisha haki ya uhuru wa dhamiri na dini kwa raia wote.
Kila mtu anasubiri uamuzi huo wa kihistoria utakaotolewa na Mahakama ya Kikatiba.