Hamia kwenye habari

Gyeong-chan Park ni mmoja kati ya wanaume 140 ambao MMAO imewatambulisha kimakosa kuwa wakwepaji wa utumishi wa kijeshi

JUNI 9, 2017
KOREA KUSINI

Mahakama ya Korea Kusini Yatambua Haki za Kibinadamu za Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Mahakama ya Korea Kusini Yatambua Haki za Kibinadamu za Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Mei 1, 2017, Mahakama ya Utawala ya Seoul ilitoa uamuzi kwamba kitendo cha Mamlaka ya Kusimamia Wanajeshi (MMAO) cha kuwaaibisha hadharani wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kama wanavyofanyiwa watu wanaokwepa utumishi wa kijeshi kunaweza kuwasababishia madhara ya kudumu. Mahakama hiyo ilitoa uamuzi kwamba MMAO haipaswi kufunua habari za kibinafsi za wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri katika tovuti yao rasmi mpaka uamuzi wa kesi ya utawala kuhusu malalamiko yaliyotolewa dhidi ya kitendo hicho cha MMAO utolewe. MMAO imekubali kutii amri hiyo ya mahakama.

Hawakwepi Utumishi wa Kijeshi

Mwanzoni mwa mwaka wa 2015, msimamizi wa MMAO alieleza kwamba habari za kibinafsi za wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zinapaswa kuwekwa hadharani kama watu wanaokwepa utumishi wa jeshi. MMAO wana habari zao kwa sababu wanaume hao wote walikuwa wametoa taarifa kwenye mamlaka hiyo (MMAO) siku moja kabla ya siku waliyopaswa kujiandikisha rasmi kwenye jeshi, wakieleza msimamo wao wa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri lakini kwamba walikuwa tayari kufanya utumishi wa badala wa kiraia. Hata hivyo, Desemba 20, 2016, MMAO ilifunua hadharani kupitia tovuti yake, majina, umri, anwani, na habari nyingine za wanaume hao kama inavyofanya kwa watu wanaokwepa utumishi wa kijeshi.

Gyeong-chan Park, ambaye ni Shahidi wa Yehova aliyekataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, alishtuka kuona jina lake ni miongoni mwa majina 237 ya watu waliokwepa utumishi wa kijeshi ambayo yaliorodheshwa kwenye tovuti. Alisema hivi: “Nimechukua msimamo kwa unyoofu wa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, na ninatarajia kwamba kutakuwa na baadhi ya watu watakaopinga msimamo wangu. Hata hivyo, nimevunjika moyo kuona serikali ikinitendea kama mtu ‘anayekwepa utumishi wa kijeshi.’ MMAO inawajua vizuri Mashahidi na sababu za kutojiunga na jeshi kwamba tunafanya hivyo si kwa sababu za ubinafsi ili kukataa kufanya utumishi kwa jamii.” Aliongeza hivi: “Ninapoona jina na anwani yangu katika orodha hiyo, ni wazi ninapata hofu sana kwamba huenda mtu fulani akaja nyumbani kwangu na kunishambulia.”

Katika ombi lao kwamba habari zao za kibinafsi zisifunuliwe hadharani, wanaume 140 ambao ni Mashahidi walioonekana katika orodha hiyo ya tovuti walieleza kwamba Sheria ya Utumishi wa Kijeshi inafafanua mtu anayekwepa utumishi wa kijeshi kuwa yule anayekataa kutii amri ya kuitwa ili kuandikishwa jeshini “bila sababu za msingi.” Wanaume hao wanaeleza kwamba wao si watu wanaokwepa utumishi wa kijeshi na pia wana “sababu za msingi” kwa kuwa sheria ya serikali ya Korea Kusini na mikataba ya kimataifa yanataka watambue haki za wale wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Uamuzi kuhusu kutambuliwa kwa haki hii nchini Korea Kusini unasubiriwa utolewe na Mahakama ya Kikatiba ya nchi hiyo.

Kutumiwa Vibaya kwa Haki ya Kufanya Uamuzi Kunaongeza Adhabu

Mashahidi wanaume wanasema kwamba kulazimika kupingwa na jamii, ingawa kunawaletea mkazo wa kiakili, na kutoheshimiwa, kumeshindwa kubadili azimio la Mashahidi wa Yehova la kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Kwa zaidi ya miaka 60 iliyopita, zaidi ya Mashahidi wa Yehova 19,000 hivi nchini Korea Kusini wamekabili mkazo huo na kuvumilia jumla ya miaka zaidi ya 36,000 ya vifungo vya gerezani. Wanaume ambao habari zao za kibinafsi zilifunuliwa wanaona hiyo kuwa njia nyingine ya kuwaadhibu na wanaona kufunuliwa hadharani kwa habari hizo ni sawa na kuweka rekodi za uhalifu ambazo serikali ya Korea Kusini inawalazimisha kuvumilia kwa sababu ya kushikamana na dhamiri zao.

Wanatarajia kwa Hamu Siku ya Kesi

Mashahidi wa Yehova nchini Korea Kusini wanafurahi kwamba mahakama imetambua suala la ukiukwaji wa haki za kibinadamu na wanatumaini kwamba uamuzi huo utakuwa na matokeo mazuri kwenye kesi yao ambayo itasikilizwa hivi karibuni na mahakama. Pia, wanataka kupeleka maombi kwenye Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Korea Kusini ili itoe maoni rasmi mahakamani kuhusu suala hili. Kesi hiyo itasikilizwa Juni 28, 2017.