Hamia kwenye habari

JUNI 16, 2014
KOREA KUSINI

Mahakimu Husumbuliwa na Dhamiri Wanapolazimika Kupuuza Dhamiri za Wengine

Mahakimu Husumbuliwa na Dhamiri Wanapolazimika Kupuuza Dhamiri za Wengine

Hakimu aliyesikiliza kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Suwon alilia alipokuwa akisoma hukumu ya kumfunga jela Chang-jo Im, mwenye umri wa miaka 21 aliyekataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Ingawa hakimu huyo alikuwa amesoma hukumu tano nyingine za wahalifu siku hiyo bila kuhuzunika, ukosefu wa haki katika kesi hiyo ulimfanya alie. Alilazimishwa na sheria kumhukumu kijana huyo ambaye ni Shahidi wa Yehova kifungo cha miezi 18.

Kila mwezi, mahakimu nchini Korea Kusini wanakabiliana na hali kama hiyo. Mwanamume kijana anapoiambia mahakama kwamba hawezi kutumika jeshini kwa sababu ya dhamiri, kwa kawaida anahukumiwa miezi 18 gerezani, bila kujali hali anazokabili. Hakimu Young-sik Kim anasema hivi kuhusu uamuzi aliofanya kuhusiana na mtu mmoja aliyekataa utumishi wa jeshi kwa sababu ya dhamiri: “Wanaposhughulika na watu wanaokataa utumishi wa jeshi kwa sababu ya dhamiri, mahakimu hawaamini kwamba ‘wanaadhibu wahalifu.’” Alisumbuliwa na dhamiri kiasi cha kwamba alitilia shaka ikiwa amri ya kujiunga na utumishi wa kijeshi inapaswa kutumiwa kuhukumu watu wanaokataa utumishi huo.

Korea Kusini inakataa kutambua haki ya watu wanaokataa utumishi wa jeshi kwa sababu ya dhamiri na haina mpango wa utumishi wa badala wa kiraia. Mahakimu nchini Korea Kusini wanalazimika kuwahukumu kama wahalifu watu wanaokataa utumishi wa jeshi kwa sababu ya dhamiri. Mahakimu wanafahamu pia kwamba Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa iliamua katika kesi nyingi, kutia ndani kesi 501 zilizohusu wanaume vijana, kwamba Korea Kusini inakiuka mkataba wake wa kimataifa wa kuheshimu haki muhimu za kibinadamu kwa kuwashtaki na kuwafunga gerezani watu wanaokataa utumishi wa jeshi kwa sababu ya dhamiri. Matokeo ni kwamba mahakimu wengi wanaendelea kusumbuliwa na dhamiri zao wanapowahukumu vijana Wakristo ambao dhamiri zao haziwaruhusu kujiunga na utumishi wa jeshi.

Kwa sasa, mahakimu sita wa mahakama za wilaya wamepeleka kesi za watu wanaokataa utumishi wa jeshi kwenye Mahakama ya Kikatiba ya Korea Kusini, ingawa mahakama hiyo ya Kikatiba iliamua hivi majuzi tu katika mwaka wa 2011 kwamba sheria ya utumishi wa jeshi inapatana na katiba. Uamuzi wa mahakimu hao pia unahusu mahangaiko mengine muhimu.

Mambo ambayo baadhi ya mahakimu wamesema kuhusu . . .

  • Uhalali wa kumfunga gerezani mtu anayekataa kuingia vitani kwa sababu ya dhamiri

    “Kusudi hasa la kuwa na sheria katika Katiba inayoonyesha kwamba uhuru wa dhamiri ni haki ya msingi, ni ili kulinda dhamiri ya mtu, kwa sababu thamani na heshima ya mwanadamu inategemea uhuru huo. . . . Ingawa uamuzi wao wa kukataa utumishi wa jeshi haupatani na maoni ya wengi, haieleweki jinsi uamuzi wao unavyolinganishwa na kosa la jinai au la uhaini hivi kwamba wastahili kuadhibiwa kama wahalifu.”–Hakimu Hye-won Lim, Mahakama ya Wilaya ya Suwon, Februari 21, 2013, 2012Chogi2381.

    “Utu wa mtu hufinyangwa kwa njia inayofaa anapoamua atakuwa na uhusiano gani na wengine . . . [na] kufikiria kwa makini ‘thamani ya uhai wa wanadamu.’ Unafinyangwa pia kwa njia hiyo anapoamua kutomuua mtu yeyote, hata kunapokuwa na vita. Ikiwa wale [ambao wamefanya] uamuzi kama huo wanalazimishwa kuingia jeshini au kulazimishwa kubeba silaha na wanaadhibiwa wanapokataa, hilo ni sawa na kuwanyima haki zao na utambulisho wao. Kwa kweli hilo linakiuka hadhi ya kibinadamu.”–Hakimu Young-hoon Kang, Mahakama ya Wilaya ya Seoul Kaskazini, Januari 14, 2013, 2012Chogi1554.

  • Ikiwa kutetea haki ya kukataa utumishi wa jeshi kwa sababu ya dhamiri kunadhoofisha usalama wa taifa

    “Hakuna ushahidi wa kutosha au habari zozote hususa zinazoonyesha kwamba kuweka mfumo wa utumishi wa badala kungehatarisha usalama wa taifa na kwamba lazima watu wafanye utumishi jeshini.”–Hakimu Gwan-gu Kim, Mahakama ya Wilaya ya Changwon Masan, Agosti 9, 2012, 2012Chogi8.

    “Hakuna sababu za kutosha kudai kwamba usalama wa taifa utahatarishwa sana kiasi cha kwamba haiwezekani kulinda hadhi ya kibinadamu na thamani ya raia wote ikiwa watu wachache tu, kutia ndani Mashahidi wa Yehova, . . . wanakataa kubeba silaha na kujifunza kuwa wanajeshi. Mshtakiwa . . . tayari amekataa kufanya utumishi wa kijeshi licha ya kuadhibiwa. Ikiwa dai hilo [lingekuwa] na msingi wowote halali, usalama wa taifa na hadhi ya kibinadamu pamoja na thamani ya raia wote tayari vingekuwa hatarini.”–Hakimu Seung-yeop Lee, Mahakama ya Wilaya ya Ulsan, Agosti 27, 2013, 2013Godan601.

  • Jinsi suala hilo linavyoweza kutatuliwa

    “Mahakama ya Kikatiba ikiamua kwamba utetezi wa washtakiwa katika kesi hiyo unapingana na Katiba, baraza la mawaziri pamoja na Bunge linaweza na linapaswa kuzingatia usalama wa taifa na uhuru wa dhamiri na basi watunge sheria zinazounga mkono kukataa utumishi wa jeshi kwa sababu ya dhamiri na wakati uleule kuimarisha usalama wa taifa.”–Hakimu Young-sik Kim, Mahakama ya Wilaya ya Seoul Kusini, Julai 9, 2013, 2013Chogi641.

    “Wanajeshi hawatakosekana na usalama wa taifa hautaathiriwa sana mradi tu mfumo wa utumishi wa badala unaundwa kwa makini ili kuzuia watu wasitumie kisingizio cha dhamiri kuwa sababu ya kutojiunga na jeshi.”–Hakimu Seong-bok Lee, Mahakama ya Wilaya ya Seoul Mashariki, Februari 20, 2014, 2014Chogi30.

Mahakama ya Kikatiba itashughulikiaje jambo hilo?

Mahakimu hao waliiomba Mahakama ya Kikatiba kutatua suala hilo linalowatatiza sana linalohusu kukataa utumishi wa jeshi kwa sababu ya dhamiri. Kwa sasa, Mahakama hiyo imeamua kwamba kesi 29 ni halali, kutia ndani kesi mbili zinazohusisha wanaume 433.

Mahakama ya Kikatiba itafanya uamuzi gani kuhusu kesi hizo? Je, Mahakama kuu zaidi nchini Korea Kusini itatambua haki ya watu wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri, na hivyo kuweka sheria mpya? Ikifanya hivyo, itaheshimu mikataba yake ya kimataifa, Katiba yake, na kuheshimu dhamiri za watu wengi na hivyo kuleta kitulizo kwa mamia ya vijana waliofungwa isivyo haki.