NOVEMBA 6, 2024
KUBA
Kimbunga Oscar Chasababisha Uharibifu Nchini Kuba
Oktoba 20, 2024, Kimbunga Oscar kilifikia maeneo yaliyo karibu na mji wa Baracoa, kwenye mkoa wa Guantánamo ulio mashariki mwa Kuba. Kimbunga hicho kilitokeza upepo uliovuma kwa mwendo wa kilomita 120 kwa saa. Upepo huo uliharibu nyaya za umeme katika eneo hilo. Baadhi ya maeneo ya mashariki mwa Kuba yalipata mvua zilizofikia kiwango cha sentimita 38 hivi na kusababisha mafuriko kwenye nyumba za watu na biashara zao, na hata kuharibu mazao. Nyumba zaidi ya 2,000 kwenye mkoa huo ziliharibiwa na watu 7 hivi walikufa.
Athari Ambazo Ndugu na Dada Zetu Wamepata
Kwa kusikitisha, dada mmoja mwenye umri mkubwa alikufa
Wahubiri 2 walipata majeraha madogo
Wahubiri 14 walilazimika kuhama makazi yao
Nyumba 13 ziliharibiwa kabisa, na 2 kati ya nyumba hizo zilikuwa zikitumiwa kufanyia mikutano
Nyumba 22 zilipata uharibifu mkubwa
Nyumba 5 zilipata uharibifu mdogo
Jitihada za Kutoa Msaada
Wawakilishi wa ofisi ya tawi, waangalizi wa mzunguko, na wazee wa eneo hilo wanatoa msaada wa kiroho na wa kimwili
Halmashauri 2 za Kutoa Msaada zinasimamia kazi ya kutoa msaada
Tunasikitishwa sana na uharibifu na vifo vilivyosababishwa na kimbunga hiki. Hata hivyo, tuna hakika kwamba Baba yetu wa mbinguni, Yehova, atawategemeza wale wanaomtegemea.—Zaburi 55:22.