DESEMBA 23, 2021
KYRGYZSTAN
Kamati ya Haki za Kibinadamu Inasema Kwamba Nchi ya Kyrgyzstan Ilikiuka Haki za Mashahidi wa Yehova
Washiriki 15 wa Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (CCPR) walishutumu kwa pamoja nchi ya Kyrgyzstan kwa kukiuka haki ya msingi ya Mashahidi wa Yehova ya kuabudu, katika maeneo matatu nchini humo. Katika hati iliyokuwa na kurasa saba, CCPR iliamuru Kyrgyzstan “iwalipe fidia” Mashahidi, na “kufanya yote iwezayo ili kuzuia ukiukaji kama huo wa haki usitokee tena.” Hii ni mara ya pili kwa CCPR kuishutumu Kyrgyzstan kwamba imekiuka haki za Mashahidi.
Kikundi cha kwanza cha Mashahidi wa Yehova nchini Kyrgyzstan kilisajiliwa mwaka wa 1993, na walisajiliwa katika taifa zima mwaka wa 1998. Basi kwa miaka mingi Mashahidi wa Yehova wamefurahia uhuru wa ibada nchini kote. Hata hivyo, kwa zaidi ya miaka kumi, Kamati ya Taifa ya Mahusiano ya Kidini (SCRA) imekataa kusajili mashirika ya kidini ya Mashahidi wa Yehova katika maeneo ya Osh, Naryn, na Jalal-Abad yaliyo Kusini mwa Kyrgyzstan. Basi katika njia hiyo SCRA imewazuia ndugu na dada katika maeneo hayo kushiriki imani yao, kuongoza mikutano ya kidini na makusanyiko, au kununua na kutumia sehemu mbalimbali kwa ajili ya ibada. Hivyo, CCPR iliamua kwamba Kyrgyzstan iliwabagua Mashahidi wa Yehova katika maeneo hayo matatu kwa msingi wa imani yao.
CCPR inatarajia kwamba wenye mamlaka nchini Kyrgyzstan watafanya “yote [wawezayo] ili kuzuia ukiukaji kama huo wa haki usitokee tena.” Kyrgyzstan ina siku 180 za kueleza CCPR mambo inayofanya ili kutekeleza uamuzi huo.
Kwa sasa hatujui ikiwa wenye mamlaka nchini Kyrgyzstan watatii uamuzi wa CCPR na kuwaruhusu ndugu na dada zetu katika maeneo hayo kutenda kulingana na imani yao. Hata hivyo, watetezi wa haki za kibinadamu wa Mkutano wa 18 (Forum 18) wamekuwa wakifuatilia hali hiyo kwa makini na wameripoti kwamba SCRA “imepuuza uamuzi mwingine kama huo uliotolewa na Umoja wa Mataifa katika mwaka wa 2019.”
Iwe Kyrgyzstan itatii uamuzi wa Umoja wa Mataifa au la, tuna uhakika kwamba Yehova anajua mambo ambayo ndugu na dada zetu nchini Kyrgyzstan wanaendelea kukabili. (Zaburi 37:18) Baba yetu wa kimbingu mwenye upendo ataendelea kuwabariki kwa sababu ya uaminifu na ujasiri wao.—Zaburi 37:28.