Hamia kwenye habari

Ndugu Stanislav Teliatnikov wa Lithuania

JUNI 15, 2022
LITHUANIA

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Yaamua Lithuania Ilikataa Kumpa Ndugu Stanislav Teliatnikov Utumishi wa Badala wa Kiraia

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Yaamua Lithuania Ilikataa Kumpa Ndugu Stanislav Teliatnikov Utumishi wa Badala wa Kiraia

Juni 7, 2022, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilitoa uamuzi ambao haukupingwa dhidi ya nchi ya Lithuania katika kesi inayomhusu Ndugu Stanislav Teliatnikov, ambaye alikataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Mahakama hiyo ilisema kwamba haki ya kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri inaungwa mkono na Kifungu cha 9 (uhuru wa kufikiri, dhamiri, na dini) cha Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu. Mahakama hiyo iliamua kwamba nchi ya Lithuania ilikuwa imekiuka Mkataba huo na ikaamuru nchi hiyo imlipe Stanislav jumla ya euro 3,000 (dola 3,196 za Marekani).

Karibu nchi zote zilizo kwenye Baraza la Ulaya zimeanzisha programu ya utumishi wa badala wa kiraia inapowezekana. Stanislav alipoagizwa ajiunge na jeshi, aliomba kufanya utumishi wa badala wa kiraia ambao unakubalika kulingana na viwango vilivyowekwa na baraza hilo. Hata hivyo, Lithuania bado haijaanzisha programu ya utumishi wa badala wa kiraia nchini humo. Katika uamuzi wa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu dhidi ya Lithuania, na pia katika maamuzi mengine kama hayo yaliyofanywa dhidi ya Armenia, Azerbaijan, na Uturuki, mahakama hiyo ilisema tena kwamba nchi zote zilizo katika Baraza la Ulaya zinahitaji kuanzisha utumishi wa badala wa kiraia, na utumishi huo haupaswi kuwa adhabu, wenye kubagua, au unaohusiana na jeshi.

Nchi ya Armenia imeanzisha mpango unaofaa wa utumishi wa badala wa kiraia. Hivyo basi, vijana ambao wanakataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri wanaweza kupewa kazi ambazo zitainufaisha jamii.

Tunatumaini kwamba nchi ya Lithuania itatekeleza mwongozo kutoka kwa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu na kuanzisha programu ya utumishi wa badala wa kiraia kwa faida ya ndugu zetu na pia jamii kwa ujumla. Huku tukisubiri hayo, tunajua kwamba Yehova ataendelea kuwapa ndugu zetu nchini Lithuania mwongozo na utegemezo wanaohitaji.​—Maombolezo 3:25.