AGOSTI 11, 2023 | HABARI ZIMEONGEZWA: SEPTEMBA 29, 2023
MAREKANI
HABARI ZA KARIBUNI—Moto Wateketeza Baadhi ya Maeneo Katika Visiwa vya Hawaii, Marekani
Agosti 8, 2023, moto uliteketeza sehemu kubwa ya kisiwa cha Maui. Kisiwa hicho ndicho cha pili kwa ukubwa kati ya visiwa vya jimbo la Hawaii, nchini Marekani. Moto huo ulisambaa haraka kwa sababu ya upepo mkali uliotokana na kimbunga kilichotokea baharini. Inasikitisha kwamba moto huo uliharibu mifumo ya mawasiliano, nyumba za watu, na hata biashara. Katika maeneo kadhaa, wenye mamlaka waliaamuru watu waondoke ili kulinda usalama wao. Imeripotiwa kwamba watu wasiopungua 97 wamekufa. Vikosi vya zima moto bado vinapambana na moto kwenye kisiwa kikubwa zaidi cha Hawaii. Hata hivyo, moto huo si mkubwa kama ule uliotokea katika kisiwa cha Maui.
Hizi ndizo ripoti za awali zilizotufikia kutoka kwa ndugu walio katika maeneo hayo.
Athari Ambazo Ndugu na Dada Zetu Wamepata
Kwa kusikitisha, ndugu 1 alikufa kutokana na mioto hiyo
Wahubiri 307 wamelazimika kuhama makao yao
Nyumba 42 ziliteketea
Nyumba 2 zilipata uharibifu mdogo
Jumba 1 la Ufalme lilipata uharibifu mdogo
Jitihada za Kutoa Msaada
Waangalizi wa mzunguko wanashirikiana na wazee wa eneo hilo ili kuwapa ndugu na dada walioathiriwa na moto huo msaada wa kimwili na kiroho unaohitajika
Halmashauri ya Kutoa Msaada imewekwa rasmi ili kusimamia jitihada za kutoa msaada
Tunatazamia kwa hamu wakati ambapo Ufalme wa Mungu utakomesha majanga ya asili ambayo yanawasababishia watu kutia ndani ndugu na dada zetu maumivu mengi katika siku hizi za mwisho.—Marko 4:39.