Hamia kwenye habari

Jumba la Ufalme lililoharibiwa na Kimbunga Dorian katika kisiwa cha Great Abaco, Bahamas

SEPTEMBA 18, 2019
MAREKANI

Kimbunga Dorian Chatokeza Uharibifu Mkubwa

Kimbunga Dorian Chatokeza Uharibifu Mkubwa

Baada ya kutokeza uharibifu katika visiwa vya Bahamas, Kimbunga Dorian kilipiga pwani ya Mashariki ya Marekani. Ijumaa asubuhi, Septemba 6, 2019, kimbunga hicho kilipita katika eneo la Cape Hatteras, North Carolina, na kutokeza mafuriko yaliyoathiri nyumba na biashara. Septemba 7, 2019, kimbunga hicho kilitokeza upepo mkali katika eneo la Nova Scotia, Kanada.

Wahubiri wa Nassau wakiwa wamekusanyika kwenye uwanja wa ndege kuwapokea ndugu na dada zao waliohamishwa kutoka kwenye Kisiwa Great Abaco

Ofisi ya tawi ya Marekani inaripoti kwamba kati ya wahubiri 1,742 katika visiwa vya Bahamas ni dada mmoja tu aliyepatwa na jeraha dogo. Kufikia wakati ambapo ripoti hii ilikuwa ikitayarishwa, jumla ya nyumba 48 za Mashahidi ziliharibika na 8 zikabomolewa.

Wahubiri wengi wanaoishi Kisiwa cha Great Abaco walihamishwa na kupelekwa Nassau, mji mkuu wa Bahamas. Walipokewa kwa uchangamfu kwenye uwanja wa ndege na ndugu na dada wa eneo hilo.

Ndugu na dada zetu wakikusanya misaada kwenye Kituo cha Makusanyiko ya Kikristo cha West Palm Beach

Halmashauri ya Kutoa Msaada na mwangalizi wa mzunguko wa eneo hilo wanaratibu utoaji wa misaada na uchungaji kwa wahubiri walioathiriwa. Pia, akina ndugu kutoka kwenye ofisi ya tawi ya Marekani wamesafiri kwenda kwenye eneo hilo ili kusaidia katika jitihada za kutoa msaada na kuandaa kitia moyo cha kiroho kwa makutaniko.

Misaada iliyosafirishwa kutoka kwenye Kituo cha Makusanyiko ya Kikristo cha West Palm Beach ikifikishwa Freeport, Bahamas. Ndugu wa eneo hilo wanapakia maboksi kwenye gari ili kuyasambaza

Nchini Marekani, kimbunga hicho kiliathiri eneo la North Carolina na South Carolina. Hakuna ndugu au dada walioathiriwa na msiba huo, lakini ndugu 737 walilazimika kuhama. Wengi kati yao wanahama kwa muda tu hadi watakapoweza tena kurudi nyumbani kwao. Pia, nyumba 50 na Majumba 12 ya Ufalme yaliharibiwa.

Hakuna ripoti inayoonyesha kwamba ndugu zetu nchini Kanada walijeruhiwa. Kimbunga hicho kilisababisha uharibifu mdogo katika baadhi ya nyumba za akina ndugu na pia kilisababisha umeme ukatike katika eneo lote. Akina ndugu na dada katika makutaniko ya eneo hilo waliwasaidia walioathiriwa.

Tunashukuru kwamba Yehova anasikiliza “sihi . . . za kuomba msaada” za ndugu zetu ambao wanamtegemea katika nyakati hizi ngumu.—Zaburi 28:6.