OKTOBA 17, 2024
MAREKANI
Kimbunga Milton Chapiga Florida, Marekani
Oktoba 9, 2024, Kimbunga Milton kiliipiga pwani ya Florida, Marekani, na kusababisha uharibifu mkubwa katika jimbo hilo. Kimbunga hicho chenye nguvu kilitokea ndani ya majuma mawili baada ya Kimbunga Helene kuipiga eneo hilo na kusababisha mafuriko na uharibifu mkubwa. Kimbunga Milton kiliambatana na upepo mkali uliosafiri kilometa 289 kwa saa. Kutokana na kimbunga hicho, baadhi ya maeneo ya pwani yalipata mvua za sentimeta 45 na dhoruba zilizofikia mita 3 zilizosababisha mafuriko makubwa.
Isitoshe, Kimbunga Milton kilisababisha uharibifu mkubwa baada ya kutokeza tufani 38 kusini na katikati mwa jimbo la Florida. Watu 80,000 hivi walibaki bila umeme, na 24 hivi wakafa.
Athari Ambazo Ndugu na Dada Zetu Wamepata
Hakuna ndugu au dada aliyekufa
Wahubiri 2 walipata majeraha makubwa
Wahubiri 4 walipata majeraha madogo
Wahubiri 9,949 walilazimika kuhama makazi yao
Nyumba 16 ziliharibiwa kabisa
Nyumba 235 zilipata uharibifu mkubwa
Nyumba 1,398 zilipata uharibifu mdogo
Jumba 1 la Ufalme lilipata uharibifu mdogo
Majumba 30 ya Ufalme hayana umeme na hayawezi kutumiwa kwa sasa
Jitihada za Kutoa Msaada
Siku mbili kabla ya Kimbunga Milton kufika kwenye nchi kavu, Ofisi ya Tawi ya Marekani ilituma barua kwa makutaniko zaidi ya 800 yaliyokuwa kwenye maeneo ambayo kimbunga hicho kingepitia. Barua hiyo ilikuwa na habari muhimu ambazo zingewasaidia wale ambao wangechagua kuondoka kwenye maeneo hayo
Waangalizi wa mzunguko na wazee wa kutaniko wanaandaa msaada wa kiroho na wa kimwili kwa ndugu na dada zetu walioathiriwa na Kimbunga Helene na Kimbunga Milton
Halmashauri 3 za Kutoa Msaada zimewekwa rasmi kusimamia kazi ya kutoa msaada kwa ajili ya vimbunga vyote viwili
Kwa upendo, mamia ya Mashahidi katika jimbo la Georgia na South Carolina, nchini Marekani, wamewaandalia makao ya muda akina ndugu na dada waliolazimika kuhama makwao
Tukiwa undugu wa ulimwenguni pote, tunasali Yehova aendelee kuwapa “kimbilio na ulinzi” wote walioathiriwa na vimbunga hivyo.—Isaya 4:6.