Hamia kwenye habari

SEPTEMBA 5, 2019
MAREKANI

Kimbunga cha Kihistoria Dorian Chapiga Bahamas

Kimbunga cha Kihistoria Dorian Chapiga Bahamas

Kimbunga Dorian, mojawapo ya dhoruba kali zaidi kuwahi kuripotiwa kwenye Bahari ya Atlantiki, kilirekodiwa kuwa kimbunga cha Category 5 katika Kisiwa cha Great Abaco kaskazini mwa Bahamas siku ya Jumapili asubuhi, Septemba 1, 2019. Dorian kilikuwa kimbunga hatari hasa kwa sababu kilikuwa kikosonga taratibu, kilikuwa na pepo zilizovuma kwa kasi, na mvua nyingi. Kimbunga hicho kilipita karibu na Kisiwa cha Leeward, Puerto Riko, na Visiwa vya Virgin kama kimbunga cha tropiki bila kusababisha madhara makubwa.

Ofisi ya Tawi ya Marekani inaendelea kukusanya habari huku wakichunguza jinsi majengo yanayomilikiwa na ofisi ya tawi na ndugu zetu walivyoathiriwa na kimbunga hicho. Wakati huohuo, hakuna majeruhi walioripotiwa kati ya wahubiri 46 katika makutaniko mawili kwenye Kisiwa cha Great Abaco. Hata hivyo, Jumba pekee la Ufalme kwenye kisiwa hicho liliharibiwa.

Kwenye Kisiwa cha Grand Bahama, kuna makutaniko manne yenye wahubiri 364. Ripoti za awali zinaonyesha kwamba ndugu zetu 196 walilazimika kuhama na nyumba 22 ziliharibiwa. Nyumba tatu ziliharibiwa kabisa.

Ofisi ya tawi iliandaa maagizo mapema kwa waangalizi wa mzunguko na wazee katika maeneo yaliyoathiriwa kuhusu kimbunga hicho. Ofisi ya tawi ilipendekeza kwamba akina ndugu wote wahamie kwenye mji mkuu wa Nassau au kwenye maeneo mengine yaliyokuwa salama.

Tunasali kwa ajili ya ndugu na dada zetu wanaoteseka kwa sababu ya kimbunga hicho. Tunajua kwamba Yehova anaelewa hali yao ngumu na ataendelea kuwapa nguvu za kukabiliana na dhiki hiyo.—Zaburi 46:1, 2.