NOVEMBA 20, 2019
MAREKANI
Moto wa Msituni Wasababisha Madhara Makubwa California
Katika miezi ya hivi karibuni, moto wa msituni ulioibuka mara kadhaa uliwaka katika jimbo la California na kuunguza karibu kilomita 362 za mraba na kuacha kovu kubwa ardhini.
Ofisi ya tawi ya Marekani imeripoti kwamba ndugu na dada zaidi ya 1,700 walihitaji kuhama makao yao kwa sababu moto huo uliwaka mara kadhaa. Hakuna mtu yeyote aliyeumia au kufa. Moto wa Sandalwood huko Calimesa ulioanza Oktoba 10, 2019, uliharibu nyumba ya ndugu mmoja. Pia baadhi ya nyumba zilipata uharibifu mdogo uliotokana na moshi. Karibu akina ndugu wote waliohama makao yao wamerudi nyumbani.
Mzee mmoja anayeishi katika moja ya maeneo yaliyoathiriwa anasema hivi: “Lazima tukazie umuhimu wa kutii mwongozo. Kwa kuwa ndugu zetu waliondoka upesi katika maeneo yaliyokuwa hatarini, hilo lilisaidia kikosi cha zima moto kuelekeza nguvu nyingi katika kuzima moto badala ya kutafuta watu.”
Waangalizi wa mzunguko pamoja na wazee wa eneo hilo wanaendelea kufanya mipango ya kusambaza mahitaji ya msingi kwa akina ndugu waliolazimika kuhama. Wahubiri walio katika maeneo ya karibu wameonyesha sifa ya ukaribishaji-wageni na kuwajali kwa upendo ndugu zao. Baada ya kujionea upendo huu mkubwa wa Kikristo ulionyeshwa, mwangalizi mmoja wa mzunguko alisema hivi, “Hatukuwa na shida yoyote kuwatafutia mahali pa kuishi wote waliohama makao yao.”
Tunamshukuru Yehova kwa wote ambao “wamekuwa chanzo cha faraja” kwa ndugu na dada walioathiriwa na moto huu wa msituni.—Wakolosai 4:11.