FEBRUARI 10, 2022
MAREKANI
Ukarabati na Ujenzi Unaendelea Kwenye Betheli ya Patterson, New York
Ujenzi wa jengo la wageni lenye orofa mbili lenye ukubwa wa mita 2,787 za mraba, unaendelea katika Kituo cha Elimu cha Watchtower cha Mashahidi wa Yehova huko Patterson, New York, Marekani. Ujenzi huo unatarajiwa kukamilishwa katikati ya mwaka 2023. Jengo hilo, litatia ndani sehemu ya maonyesho iliyo na maeneo matatu ya picha za kawaida na sehemu nyingine moja ya picha zinazobadilika kwenye skrini. Wageni 1,200 wataweza kutembelea maonyesho hayo kila siku. Mbali na hilo, majengo mengi yanafanyiwa ukarabati, na mifumo ya zamani ya majengo hayo inabadilishwa. Kufikia sasa, asilimia 40 ya ukarabati na ujenzi huo tayari umekamilika.
Ndugu wanaosimamia mradi huo wamekabili changamoto mbalimbali kutokana na janga la COVID-19. Maendeleo ya ujenzi karibu yaathiriwe na ugumu wa kupata vifaa vya ujenzi. Kwa mfano, katika kipindi fulani muhimu sana cha ujenzi, kulikuwa na upungufu wa sementi ya kutengeneza zege, lakini akina ndugu walifaulu kupata kiasi kilichohitajika ili kukamilisha sehemu kubwa ya sakafu kwa wakati. Pia, ingawa bei ya chuma ilipanda sana, akina ndugu walifaulu kupata vyuma vilivyohitajika kwa bei nafuu kwa sababu walikuwa wamefanya ununuzi mapema na walikuwa tayari wamefanya mikataba na wauzaji.
Betheli ilipofungwa kwa sababu ya janga, wajitoleaji waliendelea kufanya kazi wakiwa nyumbani, hivyo kazi ya kufanya mipango na ya usanifu haikuchelewa. Kwa muda fulani, haikuwezekana kukutana na maofisa wa eneo hilo kwa sababu ya vizuizi vilivyowekwa kwa sababu ya janga na hilo lingepunguza maendeleo ya mradi huo. Hata hivyo, halmashauri ya ujenzi ilifaulu kupata vibali vilivyohitajika kwa wakati, kwa sababu walishirikiana na idara mbalimbali za Betheli na maofisa wa serikali wa eneo hilo, kwa kutumia wajitoleaji wa nje na kwa kutumia video zilizounganishwa kwenye mtandao.
Miongozo ya kujitenga na wengine iliyobadilika-badilika, ilifanya kwa kipindi fulani isiwezekane kuwaalika wajitoleaji wapya kwenye eneo la ujenzi, na hilo lilitokeza changamoto zaidi. Lakini Septemba 2020 hivi, iliwezekana kuwaalika tena wajitoleaji wa muda wote waishi na kufanya kazi katika eneo la ujenzi.
Dada Jennifer Paul alialikwa kutumikia kwenye mradi huo wakati wa janga. Alisema hivi kuhusu kazi hiyo ya ujenzi: “Ninapenda kufanya kazi ngumu. Si eti ninapenda tu kazi yenyewe, bali ninawapenda watu wenyewe. Ninajionea tengenezo la Yehova likisonga na kujionea Yehova akiongoza mambo.”
Kwa sasa, jumla ya wajitoleaji 440, kutia ndani wafanyakazi 350 walio kwenye eneo la ujenzi, wanashughulikia ujenzi wa kituo cha wageni na miradi ya ukarabati ya Patterson. Ndugu na dada zetu wanaendelea kumwona Yehova akiandaa kila kitu kinachohitajika ili kufanikisha mradi huo.—1 Mambo ya Nyakati 29:16.
Ndugu wawili wakichimba mtaro kwa ajili ya kituo cha wageni
Dada akifanya ukarabati katika mfumo wa kupasha na kupoza joto wa jengo la udumishaji
Ndugu akijitayarisha kuinua nguzo ya chuma kwa kutumia kreni
Picha kutoka juu inayoonyesha kituo cha wageni na kituo cha elimu
Kwenye orofa ya pili ya kituo cha wageni, mjitoleaji wa ujenzi anashughulikia chuma cha kushikilia nguzo
Kreni ikitumiwa kuinua vifaa vipya vya mfumo wa kupoza joto juu ya paa la jengo la ofisi
Wajitoleaji wa ujenzi wenye furaha
Wajitoleaji wa ujenzi wakifanya kazi hadi usiku kwenye orofa ya pili ya kituo cha wageni