APRILI 23, 2020
MAREKANI
Zaidi ya Vimbunga 100 Vyasababisha Madhara Makubwa Kusini Mashariki mwa Marekani
Mfululizo wa vimbunga 100 vilipiga kusini mashariki mwa Marekani kuanzia Aprili 12 hadi Aprili 13, 2020. Huduma ya Kitaifa ya Hali ya Hewa iliripoti kwamba kimbunga kimoja kilichokuwa na upana wa kilomita tatu hivi ndicho kikubwa zaidi kuwahi kurekodiwa.
Mara moja ofisi ya tawi iliwasiliana na waangalizi wa mzunguko katika eneo hilo ili kujua ndugu zetu waliathiriwaje. Hakuna ndugu au dada aliyekufa kutokana na vimbunga hivyo. Dada mmoja alipatwa na majeraha madogo kimbunga kilipopiga nyumba yake. Kwa ujumla, wahubiri 63 walilazimika kuondoka makwao, nyumba 12 ziliharibiwa kabisa, na nyumba 58 ziliharibika kwa kadiri fulani. Mbali na hilo, Majumba matano ya Ufalme yaliharibiwa kwa kadiri ndogo na Jumba moja la Ufalme liliharibika sana baada ya kuangukiwa na mti.
Wazee na waangalizi wa mzunguko wanaendelea kuchanganua hali. Wanashughulikia mahitaji ya lazima ya kiroho na kimwili ya ndugu na dada zetu, wakiwaandalia faraja wale waliopoteza mali zao.—Isaya 40:1.