APRILI 27, 2015
MAREKANI
Dorothy Covington, Mke wa Wakili wa Hayden Covington, Afa Akiwa na Miaka 92
Dorothy Mae Sennett Covington, ambaye katika miaka ya 1940 na 1950 alikuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru wa kiraia wa Mashahidi wa Yehova, alikufa Machi 14, 2015, jijini Cincinnati, Ohio, akiwa na umri wa miaka 92.
Mstari wa Mbele Katika Kutetea Haki za Kikatiba
Katika miaka ya 1940, Dorothy alijitolea kuwa msaidizi wa wakili Victor Schmidt, Shahidi wa Yehova aliyefanya kazi ya kutetea haki za raia. Wakati huo Mashahidi wa Yehova waliteswa vikali nchini Marekani kwa sababu ya kuongezeka kwa uzalendo uliosababishwa na Vita vya Pili vya Ulimwengu. Msimamo wa Mashahidi wa kutounga mkono sherehe za kizalendo na kutojiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, kulienda kinyume kabisa na mtazamo uliokuwa umeenea wakati huo. Kitabu The Lustre of Our Country kinasema kwamba “mateso ambayo Mashahidi walikabili kuanzia 1941 hadi 1943 ndio ubaguzi mkubwa zaidi wa kidini ambao umewahi kutokea nchini Marekani katika karne ya ishirini.”
Mashahidi walishambuliwa na vikundi vya watu na kukamatwa na polisi kotekote nchini Marekani, kutia ndani Cincinnati, Ohio, na pia katika jimbo la Indiana. Victor Schmidt alisafiri katika maeneo hayo ili kutetea Mashahidi wa Yehova waliokamatwa kinyume cha sheria. Dorothy alikuwa akitegemeza kazi hiyo katika ofisi ya Victor Schmidt na wakati uleule akishiriki kwa ujasiri katika kazi ya kuhubiri licha ya vitisho vya kushambuliwa na vikundi hivyo vyenye jeuri.
Dorothy anakumbuka matukio yaliyoongoza kwenye mashambulizi ya vikundi vyenye jeuri katika eneo la Connersville, Indiana. Siku 17 tu baada ya uamuzi usio wa haki wa Mahakama Kuu wa mwaka wa 1940 katika kesi ya iliyohusu kusalimu bendera ya Minersville School District v. Gobitis, mkuu wa polisi wa Connersville aliwakamata Mashahidi sita kwa kosa la kutoiheshimu bendera kwa kukataa kusalimu pini yenye bendera ya Marekani. Katika jiji hilo la Connersville ndipo Victor Schmidt na Hayden Covington, mawakili wa Mashahidi wa Yehova kutoka mwaka wa 1939 hadi 1963, walisimamia kesi ya Mashahidi wawili kati ya hao sita walioshtakiwa baadaye kimakosa kwa kosa kupanga njama dhidi ya serikali.
Baada ya kutoa utetezi wake wa mwisho, Bw. Covington aliondoka mara moja na kusafiri ili kusimamia kesi nyingine katika jimbo la Maine, lakini Victor Schmidt na mke wake walibaki wakisubiri uamuzi wa mahakama. Baadaye, walivamiwa na kikundi cha watu wenye fujo. Victor, mke wake, na wengine walipigwa sana lakini hatimaye walifanikiwa kutoroka.
Katika mahojiano yaliyofanywa majuma matatu tu kabla ya kifo chake, Dorothy alisema kwamba miezi kumi baada ya uamuzi huo, Mashahidi 75 walifungwa jijini Connersville kwa shtaka hilohilo la uwongo la kutunga njama dhidi ya serikali. Dorothy alisema hivi: “Wakati wa matukio hayo ya Connersville, ndipo wengi wetu walikamatwa na huo ndio wakati ambapo Mashahidi walikuwa wakiteswa sana.”
Hayden Covington, Victor Schmidt, na wengine waliendelea kutetea haki za kiraia za Mashahidi wa Yehova. Covington na Schmidt walifanikiwa kubadili hukumu zilizotolewa Connersville, na Covington alimsaidia Schmidt katika kesi nyingine. Dorothy na Hayden walipokuwa wakifanya kazi pamoja walianza kuwa marafiki. Wakafunga ndoa mwaka wa 1949.
Katika Makao Makuu ya Mashahidi wa Yehova
Dorothy alihamia jijini New York ili kumsaidia Hayden katika kazi zake nyingi kwenye makao makuu ya ulimwenguni pote ya Mashahidi wa Yehova yaliyoko Brooklyn, New York, na pia aliendelea na kazi ya kuhubiri huku Hayden akiendelea na kushughulikia mambo ya kisheria. Covington aliyefahamika na wengi kuwa miongoni mwa mawakili bora zaidi wa mambo ya kikatiba wa kipindi hicho, alisimamia kwa bidii kesi nyingi zilizohusisha uhuru wa kiraia wa Mashahidi wa Yehova. Alishughulikia kesi zaidi ya 40 mbele ya Mahakama Kuu na zaidi ya kesi 100 katika mahakama za rufani.
Dorothy aliandamana na Hayden alipotetea kesi za Mashahidi wa Yehova katika Mahakama Kuu kotekote nchini Marekani. Alisema hivi: “Hayden alitetea uhuru ambao wakati mwingine tunauona kuwa wa kawaida tu. Ninafikiri inapendeza kuwa alitumia maisha yake kuwasaidia wale waliohitaji uhuru huo—si tu nchini Marekani bali pia katika maeneo mengine mengi.”
Familia na Huduma
Katika mwaka wa 1959, Dorothy na Hayden walipata binti anayeitwa Lynn, na miaka mitatu baadaye wakapata mtoto wa kiume anayeitwa Lane. Hatimaye, familia hiyo ilihama New York na kurudi Ohio mwaka wa 1972. Dorothy alitumia wakati wake kuwafundisha watoto wao Biblia na kuhubiri kwa bidii.
Hayden alikufa Novemba 21, 1978. Dorothy akarudia kazi yake ya uchapishaji kwenye magazeti mbalimbali, kutia ndani The Cincinnati Enquirer. Kazini alitumia mashine ya Linotype, na kazi hiyo ilikuwa ngumu hivi kwamba ilifikiriwa kuwa ya wanaume kwa sababu ilihusisha kuweka vipande vya madini ya risasi kwenye mashine hiyo. Alipostaafu mwaka wa 1988, Dorothy aliendelea na utumishi wa wakati wote akijitolea kufundisha watu Biblia. Alifahamika kwa kuwa mwenye bidii sana, kwa ujuzi wake mwingi wa Biblia, na uwezo wake wa kujibu maswali kwa kufungua moja kwa moja andiko linalofaa katika Biblia.
Dorothy alifiwa kwanza na mwanaye, Lane, na ameacha binti yake, Lynn Elfers, na mume wake Gary Elfers; wajukuu wawili; na mdogo wake, Ruth Sennett Naids.