Hamia kwenye habari

Juni 14, 2018
MAREKANI

Msimamo wa Ujasiri na Kufuata Dhamiri Ulianzishwa Kwenye Mahakama Kuu Miaka 75 Iliyopita

Msimamo wa Ujasiri na Kufuata Dhamiri Ulianzishwa Kwenye Mahakama Kuu Miaka 75 Iliyopita

Gathie Barnett mwenye umri wa miaka tisa na mdogo wake, Marie mwenye umri wa miaka minane, walisimama kwa heshima wakiwa kimya, wanafunzi wenzao walipokuwa wakisalimu bendera ya Marekani. Hawakujua kwamba tendo lao la imani lingewafanya wahusike katika kesi muhimu kwenye Mahakama Kuu mwaka wa 1943. Binti za Barnett waliamini kwamba wanapaswa kuapa kuwa washikamanifu kwa Mungu peke yake. Wao ni kati ya maelfu ya watoto wa Mashahidi wa Yehova ambao wamesikiliza dhamiri zao za Kikristo.—Matendo 5:29.

Kwa kuwa walichukua msimamo kwa ujasiri, Gathie na Marie walifukuzwa kutoka shule ya Slip Hill iliyoko West Virginia. Baba yao alipeleka kesi hadi Mahakama Kuu ya Marekani. Mahakama ilitoa uamuzi wake Juni 14, 1943, kwamba shule haziwezi kuwalazimisha watoto kusalimu bendera, na wakataja kwamba Mashahidi wa Yehova hawana nia ya “kuivunjia heshima bendera au nchi yao.” Kesi ya West Virginia State Board of Education dhidi ya Barnette ilitangua uamuzi wa Mahakama hiyo katika kesi ya Minersville School District dhidi ya Gobitis, ambao miaka mitatu tu awali ulikuwa umezipa shule haki ya kusisitiza kwamba wanafunzi wasalimu bendera. a

Hakimu Robert Jackson, akiandika uamuzi uliungwa mkono na 6 dhidi ya 3 katika Mahakama Kuu, alisema hivi: “Ikiwa kuna jambo lisilobadilika katika mzunguko wa kisheria, ni kwamba hakuna ofisa yeyote, hata awe na cheo gani, anayeweza kuamua ni nini kinachofaa katika siasa, nchi, dini, au jambo lingine kuhusu maoni au kuwalazimisha raia kukiri kwa neno au tendo imani yao katika mambo hayo.”

Ingawa watoto Mashahidi ndio walionufaika kwanza na uamuzi huo, Andrew Koppelman, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Northwestern, anasema hivi: “Wanaharakati wa uhuru wa raia wa Marekani wanapaswa kuwashukuru sana Mashahidi wa Yehova, ambao waliteswa vikali walipopigania uhuru wa kiraia tunaoendelea kufurahia.”

Zaidi ya kuathiri sheria za Marekani, Philip Brumley, wakili wa Mashahidi wa Yehova anaeleza hivi: “Mamlaka ya kesi ya Barnette inaweza kuonekana katika Mahakama Kuu za Argentina, Kanada, Kosta Rika, Ghana, India, Filipino, na Rwanda, pamoja na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ambazo zimenukuu kesi hiyo na kufuata majadiliano yaliyohusika.”

Mwaka wa 2006, Gathie na Marie walialikwa na kikundi cha wasomi kuzungumzia umuhimu wa kesi yao katika Kituo cha Robert H. Jackson jijini New York. Marie alisema hivi: “Ninafurahi sana kwamba watoto walioenda shuleni baada yetu walinufaika.” Gathie alisema hivi pia: “Ninakumbuka mwana wangu mkubwa alipoitwa ofisini kwa kukataa kusalimu bendera. Mkuu wa shule alisema, ‘Inaonekana mwalimu wako hakumbuki uamuzi wa Mahakama Kuu.’”

Akieleza hisia za Mashahidi wote wa Yehova, Gathie anasema: “Tunaheshimu bendera na inachowakilisha. Hatupingani na hilo. Ni kwamba tu hatuamini ni sawa kuiabudu au kuisalimu.”—1 Yohana 5:21.

a Makarani wa mahakama walikosea walipoandika majina ya watoto wa Gobita na Barnett.