SEPTEMBA 8, 2014
MAREKANI
Lillian Gobitas Klose, Mwanafunzi Aliyehusika Katika Kesi ya Kihistoria ya Mwaka 1940, Afa Akiwa na Miaka 90
NEW YORK—Lillian Gobitas Klose, ambaye uamuzi wake wa kutosalimu bendera ulimfanya ahusike katika kesi ya kihistoria iliyoendeshwa na Mahakama Kuu ya Marekani, amekufa nyumbani kwake Fayetteville, Georgia, Agosti 22, 2014. Amekufa akiwa na umri wa miaka 90.
Lillian Gobitas na mdogo wake William, ambao ni Mashahidi wa Yehova, waliamua kutosalimu bendera baada ya kusikiliza kipindi kilichotangazwa Oktoba 6, 1935 kwenye redio ya taifa, ambacho kilizungumzia kanuni za Biblia zilizopinga ibada ya sanamu. Majuma machache baadaye walifukuzwa shuleni kwa sababu ya msimamo wao. Baba yao, Walter, alipeleka kesi mahakamani ili kutetea haki za watoto wake na alishinda kesi hiyo. Bodi ya shule ilikata rufani katika Mahakama Kuu. Juni 3, 1940, Familia ya Gobitas ilishindwa kesi ya Minersville School District v. Gobitis (jina la familia hiyo liliandikwa vibaya katika rekodi za mahakama). Miaka mitatu baadaye, katika Siku ya Bendera, Juni 14, 1943, Mahakama Kuu ilibatilisha uamuzi uliofanywa katika kesi ya 1940 ya Gobitis, baada ya kufanya uamuzi wa kesi ya West Virginia State Board of Education v. Barnette, ulioruhusu watoto Mashahidi kurudi shuleni. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza katika historia ya Marekani kwa Mahakama Kuu kubatilisha uamuzi wake ndani ya kipindi kifupi cha wakati.
Novemba 2, 1923 Walter na Ruth Gobitas walimzaa Lillian Gobitas huko Minersville, Pennsylvania. Lilian Gobitas alibatizwa na kuwa Shahidi wa Yehova Machi 14, 1935. Bi. Gobitas alianza kuwa mwalimu wa Biblia wa wakati wote (Mashahidi wanawaita mapainia wa kawaida) akiwa na umri wa miaka 20, na baadaye akafanya kazi katika makao makuu ya ulimwenguni pote ya Mashahidi wa Yehova huko Brooklyn, New York, kuanzia Februari 1946 hadi Aprili 1953.
Alipokuwa akihudhuria makusanyiko ya Mashahidi wa Yehova barani Ulaya katika mwaka wa 1951, Bi. Gobitas alikutana na Erwin Klose katika ofisi ya tawi ya Mashahidi nchini Ujerumani. Waliendelea kufahamiana Bw. Klose alipokuwa akihudhuria shule ya wamishonari ya Mashahidi inayoitwa Shule ya Gileadi, iliyofanyika South Lansing, New York. Alihitimu mwaka wa 1952 na akapata mgawo wa kwenda kutumikia huko Vienna, Austria. Bi. Gobitas pia alihitimu katika shule hiyo ya wamishonari ya Mashahidi Februari 1954.
Machi 24, 1954, Lilian na Bw. Klose walifunga ndoa jijini Vienna na wakaendelea kufanya kazi ya umishonari nchini Austria. Walirudi Marekani mwishoni mwa mwaka huo kwa sababu afya ya Bw. Klose ilikuwa inazidi kuzorota kutokana na madhara aliyopata kwa kutendewa vibaya alipofungwa kwenye kambi ya mateso ya Wanazi kwa sababu ya kuwa Shahidi wa Yehova. Baadaye walipata watoto wawili, Stephen Paul na Judith Deborah. Mwaka wa 1967, familia ya Klose ilihamia Riverdale, Georgia ambako walipanua kazi ya elimu ya Biblia.
Bi. Gobitas Klose ameacha binti mmoja, Judith Klose; dada wawili, Jeanne Fry na Grace Reinisch; na ndugu mmoja Paul Gobitas. Mume wake, wazazi wake, ndugu yake William Gobitas, dada yake Joy Yubeta, na mwana wake Stephen Paul Klose walikufa kabla yake.
Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:
J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000