Hamia kwenye habari

AGOSTI 5, 2013
MAREKANI

Mashahidi Waanza Ujenzi wa Makao Makuu Mapya ya Ulimwenguni Pote Huko Warwick, New York

Mashahidi Waanza Ujenzi wa Makao Makuu Mapya ya Ulimwenguni Pote Huko Warwick, New York

NEW YORK—Mashahidi wa Yehova walianza rasmi ujenzi wa makao yao makuu mapya ya ulimwenguni huko Warwick, New York, siku ya Jumatatu, Julai 29, 2013, baada ya kupata kibali kutoka kwa wasimamizi wa jiji.

Mnamo Jumatano, Julai 17, ramani ya ujenzi ya makao makuu mapya ya Mashahidi iliidhinishwa na wote katika Kamati ya Upangaji wa Mji wa Warwick, na hicho ndicho kibali cha mwisho kilichohitajika waruhusiwe kujenga. Kibali kutoka kwa kamati hiyo kilitolewa miaka minne kamili baada ya Mashahidi kununua uwanja wa Warwick Julai 17, 2009. Baada ya kupokea kibali cha kwanza cha ujenzi Ijumaa, Julai 26, Mashahidi walianza kuchimba msingi pamoja na kufanya kazi nyingine kwenye uwanja huo, Jumatatu, Julai 29.

Sababu moja kuu iliyofanya wote katika kamati ya jiji hilo wakubali kutoa kibali hicho ilikuwa ni utayari wa Mashahidi kutumia mbinu za ujenzi ambazo haziharibu mazingira. Kwa mfano, jitihada za kuhifadhi mazingira zitatia ndani kuweka kizuizi cha kuzuia mmomonyoko wa udongo. Kizuizi hicho pia kitasaidia kuwalinda wanyama-mwitu, kama vile nyoka ambao huishi kwenye mbao, jambo litakalowazuia wasifike kwenye eneo la ujenzi.

Richard Devine, msemaji wa Mashahidi wa Yehova anaeleza hivi waziwazi: “Tunafurahi sana kuendelea kufanya kazi pamoja na maofisa wa mji wa Warwick ili kuufanikisha mradi huo. Kibali walichotupa ni hatua kubwa itakayotusaidia katika kuhamisha makao yetu makuu kutoka Brooklyn hadi Warwick.” Enrique Ford, ambaye yuko katika kamati ya ujenzi ya Mashahidi ya mradi huo pamoja na Bw. Devine, anaongezea kusema hivi: “Kupata ramani ya ujenzi tutakayotumia na kupokea kibali hicho cha pekee katika mwezi wa Julai ambacho kilituidhinisha tuanze ujenzi, ni mambo muhimu sana ambayo yatatuwezesha kumaliza mradi huu wa ujenzi katika kipindi cha miaka minne.”

Uwanja huo ulikuwa mali ya International Nickel Company kutoka mwaka wa 1960 hadi 1987 na kampuni hiyo ilikuwa imejenga makao yake makuu hapo pamoja na majengo ya kufanyia utafiti. Baada ya kukosa kutumiwa kwa miaka minne, ulinunuliwa na King’s College kwa kusudi la kujenga chuo hapo. King’s College haikufanikiwa kujenga chuo hicho. Uwanja huo ulikaa bila kutumiwa tena kwa zaidi ya miaka ishirini hadi pale Mashahidi wa Yehova walipoununua mwaka wa 2009.

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000