MEI 31, 2013
MAREKANI
Mashahidi wa Yehova Warekebisha Jumba la Kihistoria Wanalotumia Kutoa Elimu ya Biblia
NEW YORK—Baada ya marekebisho yaliyofanywa kwa miezi sita, mnamo Aprili 13, 2013, Mashahidi wa Yehova walifungua tena Jumba la kihistoria la Sinema la Stanley, lililoko Jersey City, New Jersey. Mashahidi wamelitumia jumba hilo la Stanley kwa karibu miaka 30 hivi likiwa Jumba la Kusanyiko kwa ajili ya kufundisha Biblia. Marekebisho hayo yameboresha jumba hilo lililo kituo cha elimu ya bure ya Biblia.
Viti vipya vilivyowekwa vimefanya iwe rahisi kwa watu zaidi ya 250,000 wanaohudhuria programu kila mwaka katika jengo hilo kuwa na mahali bora zaidi pa kuketi. Ukumbi mkuu na vyumba vilivyo kando yake vina mfumo wa kisasa wa video unaotumiwa hasa kwa ajili ya Lugha ya Ishara ya Marekani.
Marekebisho mengi yalifanywa hasa na Mashahidi wa Yehova waliojitolea. Wajitoleaji hao walitoka sehemu mbalimbali za Marekani ili kuboresha jengo hilo la zamani, lenye historia ya pekee.
Jumba la Sinema la Stanley limekuwapo New Jersey tangu mwishoni mwa miaka ya 1920. Ni moja kati ya majumba makubwa ya sinema yaliyowahi kujengwa nchini Marekani. Jumba hilo la kihistoria lilifungwa katika mwaka wa 1978, lakini Mashahidi wa Yehova wakalinunua katika mwaka wa 1983. Tangu lilipofunguliwa katika mwaka wa 1985, Mashahidi wamelitumia jumba hilo likiwa kituo cha elimu ya Biblia.
Akizungumzia marekebisho ya hivi karibuni ya jumba hilo, msemaji wa Mashahidi wa Yehova, J. R. Brown, anasema hivi: “Jumba la Sinema la Stanley linatumiwa hasa kama nyumba ya ibada, mahali ambapo vikundi vya watu wanaozungumza lugha zaidi ya 15 hujifunza Biblia. Jumba hilo huthaminiwa pia na wenyeji wa New Jersey, na tengenezo letu linafurahi sana kutunza historia hiyo.”
Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:
J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu. +1 718 560 5000