Hamia kwenye habari

MAREKANI

Maelezo Mafupi Kuhusu Marekani

Maelezo Mafupi Kuhusu Marekani

Historia ya Mashahidi wa Yehova nchini Marekani ilianza katika miaka ya 1870, Charles Taze Russell na wenzake walipoanzisha darasa la kujifunza Biblia. Kwa miaka kadhaa iliyofuata, walianza kutoa machapisho, wakaanzisha shirika ambalo baadaye liliitwa Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania, na pia wakafungua makao yao makuu huko Allegheny, Pennsylvania.

Mashahidi wa Yehova nchini Marekani wana uhuru wa kuabudu. Hata hivyo, mwanzoni mwa karne ya 20, walikabiliana na upinzani mkali kutoka kwa viongozi wa serikali na viongozi maarufu wa dini. Hasa katika miaka ya 1930 na 1940, Mashahidi walihusika katika kesi nyingi mahakamani. Polisi waliwakamata Mashahidi kwa sababu ya kushiriki katika kazi yao ya kuhubiri hadharani, watoto wa Mashahidi walifukuzwa shuleni kwa sababu ya kukataa kusalimu bendera, na mahakama ziliwahukumu vifungo vya gereza maelfu ya vijana Mashahidi kwa kukataa kujiunga na jeshi. Hatimaye, Mahakama Kuu ya Marekani iliwatetea Mashahidi katika masuala hayo.

Kufikia sasa, Mashahidi wameshinda kesi 50 kwenye Mahakama Kuu. Pia katika mahakama mbalimbali nchini wameshinda kesi nyingi zinazohusu mambo kama vile haki za wagonjwa, malezi ya watoto, ardhi, ubaguzi kazini, na uhamiaji. Ushindi huo umesababisha marekebisho ya sheria za katiba na kufanya uhuru wa kutoa maoni wa vyombo vya habari na dini upatikane nchini Marekani. Lakini pia ushindi huo umeleta ushawishi mzuri katika mahakama za juu za duniani kote.