Hamia kwenye habari

NOVEMBA 9, 2012
MAREKANI

Tufani Sandy Yapiga Eneo la Pwani ya Mashariki ya Marekani

Tufani Sandy Yapiga Eneo la Pwani ya Mashariki ya Marekani

NEW YORK—Mnamo Oktoba 29, 2012, Tufani Sandy ilisababisha uharibifu mkubwa katika maeneo mengi yaliyo katika mwambao wa Pwani ya Mashariki ya Marekani. Mashahidi wa Yehova wanashirikiana na wenye mamlaka ili kuwasaidia waabudu wenzao na waathirika wengine wa msiba huo.

Karibu Mashahidi 200,000 wanaoishi katika jimbo hilo wameathiriwa moja kwa moja na dhoruba hiyo. Miongoni mwa Mashahidi ambao wanaishi katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi, hakukuwa na ripoti zozote za kutokea kwa vifo bali kulikuwa na ripoti mbili za watu waliojeruhiwa kidogo. Katika jimbo la Georgia, pepo kali zilisababisha kuanguka kwa tawi la mti ambalo lilimjeruhi vibaya sana mtoto mdogo ambaye wazazi wake wanashirikiana na kutaniko la Mashahidi wa Yehova. Hadi wakati wa kutolewa kwa ripoti hii, bado mtoto huyo alikuwa katika hali mbaya. Mashahidi wa Yehova walio katika eneo liliathiriwa na wengine ambao walisikia kupitia vyombo vya habari kuhusu kujeruhiwa kwa mtoto huyo wanaendelea kuisaidia familia ya mtoto huyo.

Dhoruba hiyo imesababisha kuwe na ugumu wa mawasiliano kati ya eneo hilo na maeneo mengine. Mifumo ya mawasiliano itakaporekebishwa, ndipo itakapojulikana wazi kiwango halisi cha uharibifu.

Ripoti za awali kutoka katika Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova ya Marekani zilionyesha kwamba hakukuwa na vifo vyovyote vilivyotokea bali mtu mmoja tu alijeruhiwa kidogo katika ofisi ya tawi. Dhoruba hiyo ilisababisha uharibifu mdogo wa majengo katika makao makuu ya ulimwenguni pote ya Mashahidi wa Yehova Brooklyn, New York. Upande wa mbele wa jengo moja tu ndio ulioangushwa na pepo hizo kali, lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa na ukuta huo ulioanguka. Hakukuwa na umeme katika majengo ya ofisi ya tawi ya Patterson na Wallkill, New York, hata hivyo majengo hayo yalitumia umeme wa jenereta kwa muda fulani; lakini, bado majengo ya Warwick yanatumia umeme wa jenereta. Pia, dhoruba hiyo ilikatiza huduma za mawasiliano katika majengo hayo.

Pia, ripoti ya awali inaonyesha mambo yafuatayo: Majengo 12 ya kuabudia yanayotumiwa na Mashahidi, yanayoitwa Majumba ya Ufalme, yaliharibiwa vibaya sana na mafuriko au pepo kali; dhoruba hiyo iliharibu kwa kiasi kikubwa nyumba 219 za Mashahidi, nyumba 169 ziliharibiwa kiasi, na nyumba 710 ziliharibiwa kidogo. Vikundi kadhaa vya Mashahidi katika maeneo haya vimejipanga ili kuwasaidia waathirika na katika jitihada zao wanashirikiana na wenye mamlaka wa maeneo haya ili waweza kusaidia kutoa mahitaji ya haraka zaidi kwa waabudu wenzao na waathirika wengine.

Kwa kuwa walitarajia kwamba tufani ingefika, makutaniko ya Mashahidi wa Yehova yalihimizwa kuanza kufanya mpango wa kuhamia mahali penye usalama. Zaidi ya Mashahidi 1,100 walihamishiwa mahali penye usalama mapema kabla ya dhoruba kutokea. Mashahidi wa maeneo hayo waliwakaribisha katika nyumba zao ili kuwapatia malazi waabudu wenzao ambao walikuwa wamehamishiwa katika eneo hilo au wale ambao nyumba zao hazikuwa na umeme kwa kipindi kirefu cha wakati.

Mashahidi wanaojitolea wanafanya kazi kwa bidii ili kutosheleza mahitaji ya waamini wenzao na wataendelea kufanya hivyo kwa kadiri itakavyohitajika. “Tunawajali sana watu wote walioathiriwa na msiba huu mkubwa ,” anaeleza J. R. Brown, msemaji katika makao makuu ya Mashahidi. “Tunafurahi sana kwamba tuna nafasi nzuri ya kusaidia wengine, hasa familia yetu ya waabudu wenzetu ambao wamekumbwa na matokeo mabaya sana ya dhoruba hii kubwa. Tunawakumbuka siku zote na kusali kwa ajili yao.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu. +1 718 560 5000