Hamia kwenye habari

DESEMBA 1, 2017
MEXICO

Mashahidi Wanakaribia Kuanza Kazi Kubwa ya Kujenga Upya Nchini Guatemala na Mexico Baada ya Matetemeko ya Ardhi

Mashahidi Wanakaribia Kuanza Kazi Kubwa ya Kujenga Upya Nchini Guatemala na Mexico Baada ya Matetemeko ya Ardhi

Desemba 1 kazi kubwa ya kutoa msaada itaanza na itagharimu dola milioni 10 za Marekani. Kazi hiyo inatia ndani kujenga upya nyumba 500 hivi na Majumba ya Ufalme 16, na kurekebisha majengo mengine mengi yaliyoathiriwa na matetemeko mawili ya ardhi, yalipiga nchi ya Guatemala na Mexico mwezi wa Septemba.

MEXICO CITY—Halmashauri ya Tawi ya Amerika ya Kati itaanza kazi kubwa ya kujenga upya nchini Guatemala na Mexico Desemba 1, 2017, ikiwa sehemu ya jitihada wanazofanya za kutoa msaada baada ya matetemeko mawili ya nchi yaliyokumba eneo hilo mwezi wa Septemba. Ofisi ya tawi ilipanga kazi ya kutoa msaada mara tu baada ya matetemeko hayo, waliwaandalia ndugu zetu walioathiriwa maji, chakula, dawa, na nguo. Sehemu ya pili ya kutoa msaada itakazia fikira kujenga upya Majumba ya Makusanyiko, Majumba ya Ufalme, na nyumba za akina ndugu.

Katika majimbo ya Mexico ya Chiapas na Oaxaca, ndugu na dada 655 walilazimika kuhama baada ya tetemeko lenye ukubwa wa kipimo cha 8.2 ambalo lilitokea Septemba 7. Kazi ya kutoa msaada katika majimbo hayo mawili inatia ndani kujenga upya nyumba 315 na Majumba ya Ufalme 15. Isitoshe, majengo yanayohitaji kurekebishwa yanatia ndani nyumba 1,039, Majumba ya Ufalme 108, na Majumba ya Kusanyiko 3.

Katika jiji la Mexico City na majimbo ya Morelos na Puebla nchini Mexico, tetemeko lenye ukubwa wa 7.1-lililopiga eneo hilo Septemba 19 lilifanya ndugu na dada 463 wapoteze makao. Nyumba 158 zitajengwa upya, na nyumba 600 zinahitaji kurekebishwa pamoja na Majumba ya Ufalme, na Jumba la Kusanyiko.

Nchini Guatemala, Septemba 7 ndugu na dada 36 walipoteza makao. Katika miezi ijayo, wajitoleaji wa ujenzi kutoka nchi nyingine na wajitoleaji wa ujenzi watajenga nyumba tisa na Jumba la Ufalme. Pia, watarekebisha nyumba 20 na Majumba ya Ufalme 4.

Halmashauri ya Tawi inakadiria kwamba kazi ya kutoa msaada, ambayo inahusisha vikundi 39, itagharimu dola za Marekani milioni 10 na kazi itafanywa kwa miezi mitano hadi sita. Wajitoleaji 30 hivi wamefanya mipango ya kuhamia kwenye maeneo yaliyoathiriwa, na wengine 970 wamejitolea kusaidia kazi ya kujenga upya. Tuna uhakika kwamba Yehova atabariki kazi hiyo na roho ya kujitolea ya wote ambao “[watashiriki] katika huduma ya kutoa msaada” kwa niaba ya ndugu zetu walioathiriwa.—2 Wakorintho 8:4..

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1-845-524-3000

Guatemala: Juan Carlos Rodas +502-5967-6015

Mexico: Gamaliel Camarillo, simu +52-555-133-3048