Hamia kwenye habari

NOVEMBA 15, 2018
MEXICO

Majanga Yaliyofuatana Yapiga Mexico

Majanga Yaliyofuatana Yapiga Mexico

Oktoba 23, Mexico ilipigwa na majanga miwili ya asili, Dhoruba Vicente na Kimbunga Willa. Vicente ilisababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi katika eneo la kusini mwa Mexico ambayo yaliwaua watu 11. Kimbunga Willa kilipiga pwani ya Pasifiki ya Mexico na kusababisha mvua nyingi na upepo mkali wa kilomita 193 kwa saa, hivyo kuwalazimisha watu 4,250 wahame kutoka maeneo yaliyoathiriwa.

Ofisi ya tawi ya Amerika ya Kati, ambayo inasimamia kazi nchini Mexico, inaripoti kwamba hakuna ndugu au dada aliyekufa au kujeruhiwa wakati wa dhoruba hizo. Hata hivyo, katika jimbo la Nayarit, wahubiri 118 walihamishwa kutoka nyumbani kwao ili wakae kwenye maeneo yaliyo juu zaidi. Katika jimbo la Sinaloa, maji ya mafuriko yaliingia kwenye jumba moja la Ufalme na nyumba kadhaa za akina ndugu. Nyumba za familia tano za Mashahidi huko Michoacán pia zilikumbwa na mafuriko. Ndugu na dada wenyeji tayari wamesafisha nyumba zilizokumbwa na mafuriko na Jumba la Ufalme na kufanya marekebisho yaliyohitajiwa.

Tunasali kwamba ndugu na dada zetu nchini Mexico walioathiriwa na dhoruba hizo waendelee kuvumilia na wakumbuke tumaini la wakati ujao tulilo nalo sisi sote kwamba hakutakuwa na misiba ya asili wakati huo.—2 Wakorintho 6:4.