NOVEMBA 2, 2018
MICRONESIA
Kimbunga Yutu Kimetokeza Uharibifu Katika Visiwa vya Mariana Kaskazini
Oktoba 24, 2018, Kimbunga Yutu kilitokea katika Visiwa vya Mariana Kaskazini. Saipan na Tinian ambavyo ndivyo visiwa vikubwa zaidi viliathiriwa sana, kwani upepo unaosonga kwa zaidi ya kilomita 280 kwa saa ulibomoa nyumba na kukata umeme katika maelfu ya nyumba.
Ofisi ya tawi ya Micronesia inayosimamia kazi katika Visiwa vya Mariana Kaskazini, inaripoti kwamba hakuna ndugu na dada waliokufa au kujeruhiwa. Hata hivyo, nyumba za Mashahidi 15 ziliharibiwa kabisa na nyingine 40 zikaathiriwa kwa kiasi kikubwa. Isitoshe, makao ya wamishonari iliyoko Saipan na Majumba ya Ufalme katika visiwa vya Saipan na Tinian yaliathiriwa kidogo.
Halmashauri ya Kutoa Msaada Wakati wa Misiba inaratibu kazi ya kuwasambazia msaada walioathiriwa. Isitoshe, wahubiri waliopoteza makao yao wakati wa dhoruba wanatunzwa na Mashahidi wa eneo hilo. Mshiriki wa Halmashauri ya Tawi atasafiri kwenda kwenye eneo hilo ili kuwatia moyo walioathiriwa.
Tunasali kwa ajili ya akina ndugu wanapojitahidi kukabiliana na msiba huu wa asili. Tunafarijika kujua kwamba “Yehova yuko karibu na wote wanaomwitia,” na kwamba yeye “husikia kilio chao cha kuomba msaada.”—Zaburi 145:18, 19.