Hamia kwenye habari

AGOSTI 10, 2016
NAGORNO-KARABAKH

Nagorno-Karabakh Yamfunga Isivyo Haki Mtu Aliyekataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Nagorno-Karabakh Yamfunga Isivyo Haki Mtu Aliyekataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Artur Avanesyan, mwenye umri wa miaka ishirini anatumikia kifungo cha miezi 30 kwenye gereza la Shushi lililoko Nargorno-Karabakh licha ya kwamba alikuwa tayari kufanya utumishi wa badala wa kiraia. Mahakama zote za Nagorno-Karabakh, zimemnyima haki yake ya msingi ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Bw. Avanesyan, ambaye ni Shahidi wa Yehova, anaeleza hivi kuhusu msimamo wake thabiti wa maadili: “Dhamiri yangu hainiruhusu kufanya utumishi wa kijeshi. Ninampenda jirani yangu na sitaki kubeba silaha wala kujifunza kumdhuru yeyote.” Aliendelea kusema hivi: “Si eti najaribu kuepuka wajibu wangu wa kiraia. Niliomba nifanye utumishi mwingine wa kiraia badala ya utumishi wa kijeshi, lakini sikuruhusiwa.”

Juhudi za Kufanya Utumishi wa Badala Zazuiwa

Januari 29, 2014, Bw. Avanesyan alipokea mwito wa kuripoti kwenye Halmashauri ya Kijeshi ya Jiji la Askeran kule Nargorno-Karabakh. Siku iliyofuata alijaza fomu akieleza kuhusu kukataa kwake kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri yake na akaeleza kuhusu utayari wake wa kufanya utumishi wa badala wa kiraia. Kwa kuwa alijua kwamba nchi ya Nagorno-Karabakh haina mpango wa utumishi wa badala wa kiraia, aliamua kuomba msaada wa mwanasheria.

Kwa kuwa Bw. Avanesyan ana pasipoti ya Armenia, mwanasheria wake alikutana na maofisa nchini Armenia na vilevile nchini Nagorno-Karabakh na ikaonekana kwamba Bw. Avanesyan angeruhusiwa kufanya utumishi wa badala nchini Armenia. Ili hilo liwezekane, Bw. Avanesyan alihamia nchini Armenia. Februari 13, 2014, aliwasilisha ombi lake la kufanya utumishi wa badala kwenye Halmashauri ya Kijeshi ya Masis ya Jamhuri ya Armenia.

Kamati ya utumishi wa badala ya Armenia haikumwita Bw. Avanesyan afanye utumishi huo, badala yake Julai 14, 2014, polisi wa Yerevan, Armenia, walimwagiza afike kwenye kituo cha polisi kilichoko katikati ya jiji ambapo maofisa wa polisi kutoka Nagorno-Karabakh walikuwa wakimsubiri. Walimkamata mara moja na kumpeleka kwa nguvu kutoka Yerevan hadi mji wa Askeran, Nagorno-KarabakhWalifanya hivyo bila kuwa na agizo la mahakama, bila kumsikiliza, wala kufuata hatua zozote za kisheria.

Kukamatwa na Kesi

Julai 14, 2014, akiwa na umri wa miaka 18 tu, Bw. Avanesyan alilala katika jela kwa mara ya kwanza. Siku iliyofuata alipofikishwa mahakamani, aligundua kwamba Mahakama ya Wahalifu wa Mara ya Kwanza ya Nagorno-Karabakh, ilikuwa imetoa idhini kwamba akamatwe na kuzuiwa akisubiri kesi yake kusikizwa. Mahakama hiyo haikubadili uamuzi wake na hivyo ikamfunga Bw. Avanesyan kwenye gereza la Shushi. Rufani zote zilizokatwa kupinga uamuzi huo wa kuwekwa mahabusu kabla ya kusikilizwa kwa kesi yake zilikataliwa.

Septemba 30, 2014, Hakimu Spartak Grigoryan wa Mahakama ya Wahalifu wa Mara ya Kwanza ya Nagorno-Karabakh alimhukumu Bw. Avanesyan kifungo cha miezi 30 gerezani kwa shtaka la kuepuka utumishi wa kijeshi. a Bw. Avanesyan alikata rufani, lakini Mahakama ya Rufani na vilevile Mahakama Kuu ya Nagorno-Karabakh ziliunga mkono maamuzi ya mahakama ya mwanzo kwamba anastahili kufungwa. Atatumikia kifungo chake gerezani hadi Januari 2017.

Imara Licha ya Kutendewa Isivyo Haki

Shane Brady, mmoja wa wanasheria wake anasema hivi: “Bw. Avanesyan alizuiliwa, kukamatwa, kushtakiwa, na kufungwa kwa sababu ya kushikilia imani yake ya kidini. Licha ya kufungwa gerezani isivyo haki, bado ameazimia kushikilia kwa uthabiti msimamo wake unaotegemea dhamiri.” Bw. Brady anasema kwamba maofisa wa gereza sasa wanamruhusu Bw. Avanesyan awe na Biblia yake na machapisho yanayotegemea Biblia na pia wanawaruhusu washiriki wa familia yake wamtembelee.

Akiwa tayari amejaribu njia zote za kutafuta haki nchini mwake, Bw. Avanesyan aliwasilisha ombi kwa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR). Anatazamia itakuwa na matokeo mazuri (ingawa huenda uamuzi ukatolewa miezi kadhaa baada ya kuachiliwa kwake) kwa sababu ECHR imekuwa ikitetea haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Katika kesi ya Bayatyan v Armenia, Baraza Kuu la ECHR liliamua kwamba kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri kunalindwa na haki ya kuwa na uhuru wa kufikiri, wa dhamiri, na wa dini. Maamuzi mengine ya ECHR yamedumisha kauli hiyo. b

Maamuzi ya ECHR yamechangia kuheshimiwa kwa haki ya msingi ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri—hata katika nyakati za msukosuko au vita. Kwa mfano, katika Juni 2015, mahakama moja kuu nchini Ukrainia iliunga mkono haki ya wanaokukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kuruhusiwa kufanya utumishi wa badala wa kiraia watu wanapoandikishwa na jeshi.

Je, Kuna Tumaini kwa Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri Nchini Nagorno-Karabakh?

Mashahidi wa Yehova nchini Nagorno-Karabakh na pia ulimwenguni pote wanatumaini kwamba nchi ya Nagorno-Karabakh itatambua kwamba kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ni haki ya msingi ya kibinadamu. Je, serikali itakubali kuwapa nafasi ya kufanya utumishi wa badala wa kiraia vijana wenye amani wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri badala ya kuwafunga gerezani? Nchi ya Nagorno-Karabakh itakapotambua kwamba kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ni haki ya msingi, itajipatanisha na viwango vya Ulaya vinavyokubalika na pia itakuwa inaheshimu maamuzi manyoofu ya vijana kama Artur Avanesyan.

a Kifungo cha miezi 30 kilianza Julai 14, 2014, alipowekwa mahabusu.

b Tazama Erçep v. Turkey, na. 43965/04, 22 Novemba 2011; Feti Demirtaş v. Turkey, na. 5260/07, 17 Januari 2012; Buldu and Others v. Turkey, na. 14017/08, 3 Juni 2014.