Hamia kwenye habari

Dada Pushpa Ghimire (Kushoto) na Tirtha Maya Ghale (Kulia) wakiwa wamefungwa pamoja kwa pingu, muda mfupi kabla ya kuachiliwa huru kutoka gerezani huko Nepali Novemba 4, 2019

NOVEMBA 15, 2019
NEPAL

Mashahidi Wawili Nchini Nepali Wahukumiwa Kimakosa, Waachiliwa Kutoka Gerezani Wakisubiri Uamuzi Baada ya Kukata Rufaa

Mashahidi Wawili Nchini Nepali Wahukumiwa Kimakosa, Waachiliwa Kutoka Gerezani Wakisubiri Uamuzi Baada ya Kukata Rufaa

Novemba 4, 2019, dada wawili, Tirtha Maya Ghale na Pushpa Ghimire, waliachiliwa huru kutoka gerezani kwa masharti, ambapo tayari walikuwa wametumikia kwa zaidi ya mwezi mmoja kati ya miezi mitatu waliyopaswa kutumikia, kwa sababu tu ya kutenda kulingana na imani yao—haki inayolindwa na sheria ya Nepali na ya kimataifa.

Dada Ghale na Dada Ghimire walikamatwa mwaka mmoja uliopita kwa kosa la kuzungumza na watu ambao walipendezwa na ujumbe wa Biblia barabarani. Baada ya kushikiliwa na polisi kwa siku 13, dada hao walitozwa kiasi kikubwa kupita kiasi cha faini ya takribani dola 930 za Marekani ndipo wakaachiliwa huru. Hata hivyo, wenye mamlaka waliendelea kuwapeleleza dada hao kwa kosa la uhalifu.

Desemba 10, 2018, kesi ya uhalifu ilifunguliwa dhidi ya dada hao, na ikasikilizwa kwa miezi kumi hivi. Septemba 25, 2019, Mahakama ya Wilaya ya Rupandehi ilihukumu kila mmoja wao miezi mitatu gerezani na faini ya dola 23 za Marekani.

Hakimu wa wilaya aliona wana hatia ya kubadili imani ya watu kwa sababu tu ya kumiliki na kutoa machapisho ya kidini. Kwa kuwa Nepali ni mshiriki wa Shirika la Umoja wa Mataifa na ni moja ya nchi zilizosaini Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, serikali yao ina jukumu la kuhakikisha kwamba raia wana uhuru wa kubadilisha imani yao ya kidini na kuionyesha hadharani na faraghani. Dada Ghale na Dada Ghimire, hawakuwa wakiwalazimisha watu wabadili dini zao, bali waliwapatia machapisho ya kidini wale waliokuwa tayari kuwasikiliza. Kwa msingi huo, mawakili waliowawakilisha dada hao walikata rufaa kwenye Mahakama Kuu Oktoba 31, 2019. Mahakama Kuu iliamua kwamba dada hao hawakupaswa kubaki gerezani katika kipindi hicho cha rufaa, hivyo waliachiliwa huru huku wakisubiria uamuzi wa mwisho wa mahakama.

Tunasali kwamba Yehova aendelee kuwapa roho yake takatifu dada Ghale na dada Ghimire, itakayowapa nguvu, shangwe, na amani wanapoendelea kusubiria uamuzi wa mwisho baada ya kukata rufaa.—Waroma 15:13.