Hamia kwenye habari

Jengo lililojaa maji ya mvua katika Jimbo la Rivers

OKTOBA 21, 2022
NIGERIA

Mafuriko Makubwa Nchini Nigeria Yasababisha Janga “Kubwa Kupindukia”

Mafuriko Makubwa Nchini Nigeria Yasababisha Janga “Kubwa Kupindukia”

Kumekuwa na mvua kubwa kupita kiasi nchini Nigeria nayo imesababisha mafuriko makubwa. Kwa miaka mingi, hakujawa na mafuriko kama hayo. Maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni yale yaliyo pembezoni mwa Mto Niger na Mto Benue pamoja na maeneo ya pwani ya kusini ya nchi hiyo. Mafuriko hayo yameharibu miundo-mbinu, yamewalazimu watu zaidi ya milioni moja kuhama makao yao, na yamesababisha vifo vya watu 600 hivi. Shirika la Kitaifa la Kushughulikia Dharura nchini Nigeria limesema kwamba hilo ni janga “kubwa kupindukia.” Wenye mamlaka wanaamini kwamba kutakuwa na uhaba wa chakula kwa sababu mafuriko hayo yamesababisha uharibifu katika eneo kubwa sana.

Athari Ambazo Ndugu na Dada Zetu Wamepata

    Ndugu akihama eneo lililojaa maji ya mvua

  • Hakuna ndugu au dada yetu aliyeuawa

  • Wahubiri 4,074 wamelazimika kuhama makao yao

  • Nyumba 900 zimejaa maji

  • Nyumba 180 zimeharibiwa kabisa

  • Jumba 1 la Kusanyiko pamoja na Majumba 70 ya Ufalme yamejaa maji

Jitihada za Kutoa Msaada

  • Halmashauri 4 za Kutoa Msaada zimeanzishwa

  • Wahubiri waliolazimika kuhama makao yao wanapewa chakula, makao ya muda, na mahitaji mengine ya msingi

  • Wazee wa eneo hilo wanashirikiana na waangalizi wa mzunguko ili kuwafanyia ziara za uchungaji na kuwapa msaada unaohitajika wale walioathiriwa na janga hilo

  • Jitihada zote za kutoa msaada zinafanywa kwa kupatana na miongozo ya usalama ya kujilinda na COVID-19

Tunafarijiwa kujua kwamba licha ya nyakati ngumu tunazopitia, Yehova anaendelea kuwaandalia watu wake mahali pa kuishi katika “siku ya msiba.”​—Zaburi 27:5.