Hamia kwenye habari

Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Oslo

JANUARI 11, 2023
NORWAY

Mahakama Nchini Norway Yakubali Kusimamisha Kuondolewa kwa Usajili wa Mashahidi wa Yehova

Mahakama Nchini Norway Yakubali Kusimamisha Kuondolewa kwa Usajili wa Mashahidi wa Yehova

Desemba 30, 2022, Mahakama ya Wilaya ya Oslo ilikubali ombi lililowasilishwa na ndugu zetu wakiomba mahakama itoe amri ya kusimamisha kwa muda jaribio la serikali la kuwaondolea Mashahidi wa Yehova usajili wa kisheria unaowatambua kuwa jamii ya kidini nchini Norway. Ndugu zetu walienda mahakamani kwa sababu Gavana wa Jimbo la Oslo na Viken alitangaza kwamba alikuwa ameamua kufutilia mbali usajili wetu nchini humo. Agizo lililotolewa na mahakama linatuwezesha kuendelea kutambuliwa kisheria huku tukisubiri suala hilo lichunguzwe zaidi na mahakama. Hata hivyo, Wizara ya Watoto na Familia inapinga agizo hilo la mahakama.

Ofisi ya utafsiri ya Norway pamoja na majengo ya shule ya kitheokrasi. Majengo hayo yalitumiwa yakiwa ofisi ya tawi ya Norway hadi mwaka wa 2012 ambapo kazi nchini Norway ilianza kusimamiwa na ofisi ya tawi ya Skandinavia, iliyoko Denmark

Amri hiyo ya mahakama imeleta manufaa ya moja kwa moja kwa ndugu zetu kutia ndani wachumba ambao wamepanga kufunga ndoa. Norway inawaweka rasmi wasajili wa ndoa kutoka tu katika dini ambazo zimeandikishwa kisheria nchini humo. Serikali ilipotangaza kwamba itafuta usajili wa Mashahidi wa Yehova, hilo lilimaanisha kwamba wasajili wa ndoa ambao ni Mashahidi hawangetambuliwa tena na serikali na hawangekuwa na mamlaka yoyote. Hata hivyo, amri ya mahakama sasa inaruhusu wachumba kufunga ndoa kwenye Jumba la Ufalme na kuwa na Shahidi wa Yehova ambaye atafungisha ndoa yao.

Ndugu Bjørnstad na Dada de Andrade Montelo, ambao ni wachumba. Maelezo yao yalitiwa katika kesi iliyowasilishwa Desemba 28, 2022

Ndugu André Bjørnstad na Dada Yasmin de Andrade Montelo ni miongoni mwa wachumba ambao wamepanga kufunga ndoa ambao waliathiriwa moja kwa moja. Maelezo yao yalitiwa ndani kwenye kesi iliyowasilishwa Desemba 28, 2022. Ndugu Bjørnstad alikiri kwamba huenda wengine wasielewe kwa nini yeye na mchumba wake walitaka sana Shahidi wa Yehova afungishe ndoa yao. Anaeleza: “Imani na itikadi ni mambo muhimu sana. Mambo hayo yasipoheshimiwa, unahisi ni kana kwamba unapoteza sehemu ya utambulisho wako.”

Kabla ya serikali ya Norway kuamua kuondoa usajili wa Mashahidi wa Yehova, walikuwa wamekataa kutupatia utegemezo wa kifedha ingawa tulikuwa tumepewa msaada huo kwa zaidi ya miaka 30. Serikali hugawa msaada huo wa kifedha kwa zaidi ya dini 700 ambazo zimesajiliwa kisheria nchini humo. Desemba 21, 2022, Mashahidi wa Yehova walifungua kesi dhidi ya serikali ya Norway, wakipinga uamuzi wa serikali hiyo wa kukataa kuwapa utegemezo wa kifedha.

Serikali ya Norway haikubaliani na imani yetu inayotegemea Maandiko kuhusu kutenga na ushirika. Gavana hata alisema kwamba Mashahidi wa Yehova wanapaswa kubadili imani yao kuhusu kutenga na ushirika ikiwa wanataka kuendelea kusajiliwa kisheria. Matendo hayo dhidi ya Mashahidi wa Yehova hayategemei maoni yoyote ya wataalamu au maamuzi ya mahakama.

Gavana alisema kuondolewa kwa usajili wa kisheria hakumaanishi kuondolewa kwa uhuru wa kidini. Hata hivyo, katika kesi nyingine kama hizo zinazohusisha kukataa kusajili shirika letu kisheria, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ilitoa uamuzi uliosema kwamba kufanya hivyo ni kukiuka uhuru wa kidini wa Mashahidi wa Yehova. a

Ndugu Jørgen Pedersen, mshiriki wa Halmashauri ya Tawi ya Skandinavia, anasema: “Mashahidi wa Yehova wameabudu kwa uhuru nchini Norway kwa zaidi ya miaka 130. Uhuru na haki zetu za msingi zinalindwa na Katiba ya Norway na Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu. Ikiwa mahakama za Norway zitatuunga mkono, hilo litaimarisha haki na uhuru wa raia wote nchini Norway.”