Hamia kwenye habari

Wamishonari wa kwanza waliotumika nchini Peru. Safu ya nyuma (kushoto hadi kulia): Evelyn Berry, Verda Pool, Walter Akin, Nellena Pool, and Hazel Trim

Safu ya mbele (kushoto hadi kulia): Gwendolyn Patterson, Robert Patterson, and Christine Akin

DESEMBA 2, 2021
PERU

Kwa Miaka Sabini na Tano Peru ‘Yachanua Kama Waridi’

Kwa Miaka Sabini na Tano Peru ‘Yachanua Kama Waridi’

Wamishonari wa kwanza waliopewa mgawo nchini Peru, walifika Oktoba 1946. Wamishonari hao walikuwa wamepata eneo kubwa la kuhubiri. Kulikuwa na watu milioni saba hivi walioishi katika eneo hilo lenye mandhari tofauti-tofauti, lenye ukubwa wa kilomita za mraba takriban milioni 1.3. Kwa miaka 75 iliyopita, wamishonari na wahubiri wenyeji wamefanya kazi kwa bidii, katika vijiji vilivyo milimani na hata miji iliyo pwani na watu wengi wamejifunza kweli.

Miaka kadhaa kabla ya wamishonari kufika, Mashahidi wa Yehova kutoka Amerika Kusini, walitembelea Lima, jiji kuu la Peru, na kuwapa watu waliopendezwa machapisho. Baadhi ya watu hao waliamua kumtumikia Yehova. Mwaka wa 1945, wamishonari wawili waliokuwa wakitumikia nchini Chile, walisafiri hadi Lima na kuwabatiza watu watatu na watu hao wakawa Mashahidi wa Yehova wa kwanza nchini Peru.

Kuanzia Oktoba 1946 na kuendelea, wamishonari kutoka Gileadi walipewa mgawo wa kupanga kazi nchini Peru. Walifanya mkutano wao wa kwanza katika wilaya ya Rimac iliyo Lima pamoja na watu waliopendezwa. Kadiri idadi ya wahubiri wenyeji na idadi ya wamishonari ilivyozidi kuongezeka, basi walianza kuhubiri katika maeneo mengine zaidi ya Lima. Kazi ya kuhubiri inaendelea katika maeneo mengine hata sasa.

Sister Nellena Pool

Dada Nellena Pool, mmoja wa wamishonari waliofika katika mwaka wa 1946, alizungumzia ongezeko nchini Peru katika simulizi la maisha yake, lililochapishwa katika gazeti Mnara wa Mlinzi la Machi 1, 1957. Alisema: “Ni vigumu kueleza jinsi nilivyohisi nilipoona nchi ambayo ilikuwa jangwa, ikianza ‘kuchanua kama waridi.’”

Dada Irene Mannings, mhitimu wa darasa la 54 la Gileadi, ambaye bado anatumikia nchini Peru, anasema: “Tangu tulipowasili, tumeona jinsi idadi ya wahubiri ilivyoongezeka, kutoka wahubiri 7,000 hadi wahubiri zaidi ya 130,000. Nimefurahia mchango wangu mdogo katika ukuzi huo. Yote hayo yamewezekana kwa sababu ya baraka za Yehova.”

Wahubiri 133,170 wanaotumikia sasa nchini Peru, wanathamini sana msingi mzuri wa kiroho uliowekwa miaka 75 iliyopita. Historia ya Mashahidi wa Yehova nchini Peru, ni uthibitisho mwingine wa utimizo wa ahadi ya Yehova katika Isaya 60:22: “Mdogo atakuwa elfu na mnyonge atakuwa taifa lenye nguvu.”