Hamia kwenye habari

MEI 6, 2016
RWANDA

Jamhuri ya Rwanda Yazingatia Utekelezaji wa Sheria

Jamhuri ya Rwanda Yazingatia Utekelezaji wa Sheria

Kupitia jitihada za Mchunguzi Maalumu wa Malalamiko ya Wananchi wa Rwanda na mahakimu walio makini, Mashahidi wa Yehova wamepata haki yao baada ya pambano la kisheria la muda mrefu. Mwanzoni Mahakama Kuu ya Taifa iliwahukumu Mashahidi wa Yehova na kuwaamuru walipe fidia kwa mmiliki wa jengo ambalo maofisa wa jiji la Kigali waliagiza libomolewe. Hata hivyo, Mchunguzi huyo Maalumu aliona wazi ukosefu huo wa haki na kuiomba Mahakama Kuu ya Taifa ichunguze upya uamuzi wake.

Maofisa wa Jiji la Kigali Waagiza Jiji Lisafishwe

Ikiwa ni mwanzo wa kampeni ya kusafisha jiji, mwaka 2006 maofisa wa jiji la Kigali walitoa amri kwa wakazi wote wa jiji waondoe vibanda vyote vya biashara vilivyojengwa kwenye maeneo ya umma. Isitoshe, amri hiyo ilihusisha pia kudumisha na kuyarembesha maeneo ya umma yanayozunguka maeneo ya wakazi wa jiji hilo.

Amri hiyo ilitia ndani pia kubomolewa kwa majengo yaliyojengwa kinyume cha sheria. Mojawapo lilikuwa ni jengo la Bw. Ngayabateranya ambalo lilijengwa kwenye eneo la umma bila ruhusa. Isitoshe, alitumia vifaa na njia za ujenzi zisizokidhi viwango vilivyowekwa. Siku 21 za kutekeleza agizo hilo zilipopita bila hatua yoyote kuchukuliwa, meya wa Wilaya ya Gasabo alitoa amri ya maandishi ya kubomoa majengo yote yaliyojengwa kinyume cha sheria. Baada ya majengo kuondolewa kwenye maeneo ya umma, ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova, ambayo ipo Wilaya ya Gasabo kwenye Eneo la Remera jijini Kigali, iliamua kurembesha eneo la umma lililokuwa karibu na majengo yao kwa kutengeneza njia na kupanda bustani.

Mahakama ya Wilaya Yawahukumu Mashahidi

Baada ya maofisa wa jiji kubomoa jengo la Bw. Ngayabateranya, yeye na wenzake waliamua kufungua mashtaka dhidi ya Mashahidi wa Yehova kwenye Mahakama ya Wilaya ya Gasabo wakiwatuhumu Mashahidi kwamba ndio waliobomoa jengo hilo. Bw. Ngayabateranya na wenzake walisisitiza kwamba walihitaji kulipwa fidia kwa sababu ya kubomolewa kwa jengo lao hata ingawa hawakutoa ushahidi unaoridhisha wa kuthibitisha madai yao. Mashahidi wa Yehova walitoa hati zinazothibitisha wazi kwamba maofisa wa jiji ndio wanaopaswa kuwajibika kutokana na uharibifu huo. Hata hivyo mahakama hiyo ilikataa uthibitisho huo na kuwahukumu Mashahidi kuwa na makosa.

Mahakama Kuu ya Jamhuri Yafanya Uamuzi Tofauti

Mashahidi wa Yehova walikata rufaa kwenye mahakama kuu ya Jamhuri ili kushughulikia ukosefu huo wa haki. Baada ya kuipitia kesi hiyo, mahakama hiyo iligundua kwamba hukumu iliyotolewa na mahakama ya wilaya haikuwa na msingi wowote. Novemba 5, 2010, mahakama kuu ya Jamhuri ilieleza kwamba Bw. Ngayabateranya na wenzake walifungua kesi isiyo na maana na kuwaamuru walipe faranga 800,000 za Rwanda ambazo ni sawa na dola 1,360 za Marekani ili kulipia gharama mbalimbali zilizotumika wakati wa kesi hiyo.

Mahakama Kuu ya Taifa Yakosa Uthibitisho Muhimu

Bw. Ngayabateranya alikata rufaa kwenye Mahakama Kuu ya Taifa ya Rwanda. Wakati kesi ikiendelea, Katibu Mkuu wa serikali wa Eneo la Remera alithibitisha kwamba jengo la Bw. Ngayabateranya lilijengwa kinyume cha sheria na hivyo kubomolewa kwake ni sehemu ya mpango wa Taifa wa kurekebisha jiji. Mahakama Kuu ya Taifa ilitambua wazi kwamba Mashahidi wa Yehova hawakuhusika hata kidogo na tukio la kubomolewa kwa jengo hilo. Hata hivyo, mahakama hiyo ilieleza kwamba Mashahidi ndio waliochochea kubomolewa kwa jengo hilo. Mahakama hiyo ilipuuza uthibitisho wa maana uliotolewa na kisha ikaeleza kwamba Mashahidi walinufaika isivyo haki kwa sababu walirembesha eneo ambalo awali lilikuwa na jengo lililobomolewa. Mahakama iliagiza walalamikaji walipwe faranga za Rwanda 22,055,242 ambazo ni sawa na dola 33,000 za Marekani kufidia uharibifu uliotokea. Aprili 4, 2013 Mashahidi walilipa gharama hizo huku wakiwa wameweka pingamizi katika maamuzi hayo.

Mchunguzi Maalumu Ahimiza Mahakama Kuu ya Taifa Irekebishe Ukosefu wa Haki

Mashahidi wa Yehova walipeleka malalamiko yao kwenye Ofisi ya Mchunguzi Maalumu wa Malalamiko ya Wananchi kwa sababu walishtakiwa kimakosa na kubebeshwa isivyo haki shutuma ya kuchochea kubomolewa kwa jengo la Bw. Ngayabateranya. Mchunguzi Mkuu wa Malalamiko nchini Rwanda, Bi. Aloysie Cyanzayire, alichunguza upya malalamiko hayo pamoja na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Taifa.

Baada ya kuchunguza uthibitisho, Bi. Cyanzayire alithibitisha kwamba jiji lilibomoa jengo la Bw. Ngayabateranya kwa sababu alishindwa kufuata sheria za ujenzi za Rwanda. Pia, alikiri kwamba hakukuwa na sababu ya kuwaadhibu Mashahidi kwa kuunga mkono mpango wa jiji wa kurembesha maeneo ya umma yanayowazunguka. Mashahidi wamekuwa “msaada mkubwa” kwa kuendelea kudumisha eneo hilo na “wananufaisha taifa kwa kuunga mkono mpango wake wa kulisafisha jiji.”

Majengo yaliyojengwa kinyume cha sheria kabla ya kutolewa amri ya kuyabomoa jijini Kigali na jinsi maeneo ya umma yanavyoonekana baada ya majengo hayo kubomolewa

Desemba 4, 2013, Bi. Cyanzayire aliiomba Mahakama Kuu ya Taifa ichunguze upya uamuzi wake dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Jopo jipya la majaji liliundwa ili kusikiliza kesi, na Oktoba 17, 2014, Mahakama ilisikiliza upya kesi hiyo na kutambua kwamba malalamiko ya Bw. Ngayabateranya hayakuwa na msingi. Ilimwamuru Bw. Ngayabateranya arudishe pesa alizopokea isivyo haki kutokana na uamuzi uliopita wa mahakama na alipe gharama za kesi. Wakili wa Mashahidi wa Yehova pamoja na afisa wa mahakama wanashughulikia kurudishwa kwa pesa hizo.

Kulindwa na Sheria

Mashahidi wa Yehova wangependa kutanguliza shukrani zao za dhati kwa msaada waliopata kutoka kwa Bi. Cyanzayire ambaye ni Mchunguzi Maalumu wa Malalamiko ya Wananchi na pia wanaishukuru Mahakama Kuu ya Taifa kwa kukubali kusikiliza upya kesi yao. Bila shaka raia wote wanaotii sheria wanafurahi kwamba Jamhuri ya Rwanda ina mpango madhubuti wa kushughulikia ukosefu wa haki na inazingatia utekelezaji wa sheria.