Hamia kwenye habari

JULAI 2, 2015
RWANDA

Mahakama ya Rwanda Yapinga Ubaguzi wa Dini

Mahakama ya Rwanda Yapinga Ubaguzi wa Dini

Mahakama ya wilaya ya Karongi nchini Rwanda imetetea haki ya uhuru wa ibada ya wanafunzi nane ambao ni Mashahidi wa Yehova. Wanafunzi hao walishtakiwa kwa kosa la kukataa kushiriki vipindi vya dini shuleni.

Shule nyingi nchini Rwanda zinashirikiana na mashirika ya dini. Baadhi ya shule hizo zinawalazimisha wanafunzi washiriki kwenye vipindi vya dini na kulipa ushuru wa kanisa. Kwa kuwa wanafunzi ambao ni Mashahidi wa Yehova wamekataa kufanya hivyo, wanafunzi 160 kutoka shule mbalimbali nchini Rwanda wamefukuzwa na uongozi wa shule kuanzia mwaka 2008 hadi 2014. Ingawa hilo ni tatizo la nchi nzima, uamuzi uliotolewa na mahakama ya Karongi, katika Jimbo la Magharibi, unaonyesha kwamba serikali ya Rwanda inaweza kukomesha ubaguzi wa dini.

Ubaguzi wa Dini Unasababisha Wanafunzi Wafukuzwe Shule

Mei 12, 2014, uongozi wa shule ya Groupe Scolaire Musango iliyopo Karongi, uliwafukuza wanafunzi nane ambao ni Mashahidi wa Yehova, wenye umri wa kati ya miaka 13 hadi 20 a kwa kosa la kukataa kushiriki kipindi cha dini. Walipofukuzwa, wazazi wao walitoa taarifa kwa Katibu Mtendaji wa Eneo la Rwankuba, ambaye aliagiza wanafunzi hao warudishwe shuleni. Wakiwa hawajaridhika na uamuzi huo, viongozi wa shule walitumia mbinu nyingine na kuwashtaki wanafunzi hao kwa kudharau wimbo wa taifa kwa kuwa walikataa kuimba wimbo huo. Juni 4, 2014, siku mbili tu baada ya wanafunzi hao kuanza masomo, polisi walifika shuleni hapo na kuwakamata.

Polisi waliwaweka mahabusu wanafunzi hao kwa siku sita. Maofisa wa polisi waliwatisha na kuwatukana, pia waliwapiga wanafunzi wawili ambao walikuwa na umri mkubwa kwa madai ya kuwashawishi wale wadogo. Licha ya kutendewa isivyo haki, wanafunzi wote nane walikataa kukana imani yao.

Mahakama Yawaweka Huru Wanafunzi

Juni 9, 2014 polisi waliwatoa mahabusu wanafunzi saba, na mwendesha mashtaka alimfutia mashtaka mwanafunzi mwenye umri mdogo zaidi. Hata hivyo, polisi waliendelea kumshikilia mwanafunzi mwenye umri mkubwa kwa siku tisa zaidi. Hakimu aliamuru mwanafunzi huyo aachiliwe kwa muda chini ya uangalizi wa mahakama, na akaahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 14, 2014.

Kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea kusikilizwa, hakimu alimuuliza maswali kila mwanafunzi. Alipokuwa akizungumza kwa niaba ya wenzake, mwanafunzi mmoja alimwambia hakimu kwamba kosa lililofanya wafukuzwe shule si kukataa kuimba wimbo wa taifa bali ni kukataa kulipa ushuru wa kanisa na kushiriki vipindi vya dini shuleni hapo.

Hakimu alimwagiza mwendesha mashtaka atoe ushahidi zaidi unaothibitisha kwamba wanafunzi hao “walidharau wimbo wa taifa.” Mwendesha mashtaka alipowashinikiza watoe habari zaidi, wanafunzi hao walisema waziwazi kwamba hawakuonyesha dharau wenzao walipokuwa wakiimba wimbo wa taifa.

Katika maandishi ya uamuzi uliotolewa Novemba 28, 2014, hakimu wa mahakama ya Karongi alibainisha wazi kwamba kutoimba wimbo wa taifa “hakupaswi kuonwa kuwa tendo la kukufuru au dharau.” Hatua ya mahakama hiyo kuzingatia sheria na kuwaweka huru wanafunzi hao, kutasaidia kukomesha ubaguzi wa dini kwenye shule zote nchini Rwanda.

Waomba Haki za Msingi Ziheshimiwa

Mashahidi wa Yehova nchini Rwanda wanashukuru sana kwamba matokeo ya kesi ya wanafunzi wa shule ya Groupe Scolaire Musango yalikuwa mazuri. Hata hivyo, katika visa vingine watoto wa Mashahidi wa Yehova waliofukuzwa shule kwa sababu ya imani yao wamelazimika kuhamia shule nyingine. Watoto wengine wameshindwa kuendelea na masomo kwa sababu familia zao hazina uwezo wa kuwapeleka shule za watu binafsi.

Kama wazazi wengine, wazazi Mashahidi wanapenda watoto wao wasome. Wanataka watoto wao wajifunze stadi za maisha ili wawe raia wenye manufaa kwa jamii. Mashahidi wa Yehova wanatumaini kwamba uamuzi uliotolewa na mahakama ya Karongi utasaidia shule zote nchini Rwanda ziheshimu haki ya watoto ya kuwa na uhuru wa dhamiri na kuabudu.

a Nchini Rwanda, mtoto ni mtu yeyote aliye chini ya umri wa miaka 21 (Kifungu cha Sheria ya raia namba 360).