Hamia kwenye habari

SINGAPORE

Wamefungwa kwa Sababu ya Imani Yao​—Singapore

Wamefungwa kwa Sababu ya Imani Yao​—Singapore

Vijana nane ambao ni Mashahidi wa Yehova wamefungwa nchini Singapore kwa kuwa walikataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Ndugu watatu kati yao wamehukumiwa kwa mara ya pili kwa kukataa kubadili msimamo wao baada ya kutumikia vifungo vyao vya kwanza. Vijana hawa hawana nafasi ya kufanya utumishi wa badala nchini Singapore kwa kuwa serikali inawalazimisha watu kujiunga na utumishi wa kijeshi na haitambui haki ya wale wanaokataa kujiunga na utumishi kwa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

Shahidi mwanamume anapofikisha umri wa miaka 18, sheria inamlazimisha kujiunga na jeshi la Singapore. Akikataa kwa sababu ya dhamiri, anazuiliwa kwenye kambi ya kijeshi kwa muda unaoweza kufikia miezi 12 hivi. Mwishoni mwa kipindi hicho, anaweza kupata uhuru kwa kuzoezwa kuwa mwanajeshi, hivyo anaamrishwa avae sare za kijeshi. Akikataa tena, anazuiliwa mara ya pili kwa kipindi kinachoweza kufikia miezi 18 hivi chini ya sheria za kijeshi. Hivyo, vijana hao ambao ni Mashahidi wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri wanalazimika kutumikia kifungo cha gerezani kwa awamu mbili kwa jumla ya miezi 30.

Singapore Imekataa Kutii Maagizo ya Umoja wa Mataifa

Shirika la Umoja wa Mataifa limeendelea kuhimiza mataifa yaliyo chini ya muungano huo “kutambua kwamba kukataa kujiunga na jeshi ni mojawapo ya njia ambazo mtu huonyesha kwamba ana haki ya uhuru wa kufikiri, dhamiri, na dini, na ambazo hutambuliwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu.” Ingawa nchi ya Singapore imekuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa tangu 1965, imesema kwamba haikubaliani na Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala hilo. Aprili 24, 2002, ofisa mmoja wa serikali ya Singapore aliijibu Tume ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa kwa kusema “matendo au imani ya mtu yanapopingana [na haki ya ulinzi wa taifa], haki ya serikali ya kudumisha usalama wa taifa lazima itangulizwe.” Ofisa huyo aliandika hivi waziwazi: “Hatukubali kwamba haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri inaweza kutumika katika mataifa yote.”

Mfuatano wa Matukio

  1. Agosti 16, 2024

    Jumla ya Mashahidi nane wa Yehova wako gerezani kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

  2. Aprili 24, 2002

    Ofisa wa serikali anakiri kwamba Singapore haitambui haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

  3. Februari 1995

    Kuongezeka kwa ukandamizaji na kukamatwa kwa raia wa Singapore ambao ni Mashahidi wa Yehova.

  4. Agosti 8, 1994

    Mahakama Kuu ya Singapore yafutilia mbali rufaa ambayo Mashahidi walikata.

  5. Januari 12, 1972

    Serikali ya Singapore yafutilia mbali kusajiliwa kisheria kwa Mashahidi wa Yehova.