Hamia kwenye habari

JULAI 8, 2016
SRI LANKA

Mashahidi Watoa Msaada Baada ya Mafuriko Nchini Sri Lanka

Mashahidi Watoa Msaada Baada ya Mafuriko Nchini Sri Lanka

COLOMBO, Sri Lanka—Katika milima ya Aranayaka, Sri Lanka, eneo lililo kilomita 100 hivi nje ya mji mkuu, Colombo, mvua kubwa zilisababisha maporomoko ya ardhi katika vijiji kadhaa. Zaidi ya watu 100 walikufa na 350,000 hivi wakaathiriwa. Mvua hizo zilizosababisha maporomoko hayo zilianza kunyesha kuanzia Mei 15, na pindi fulani katika muda wa saa 24 kiasi cha milimita 373 kilimwagika katika mji wa Kilinochchi. Wenye mamlaka wanasema kwamba huu ndio msiba mbaya zaidi wa asili kuipiga Sri Lanka tangu tsunami ya mwaka wa 2004.

Kulingana na ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Sri Lanka, hakuna Shahidi aliyekufa katika msiba huo, lakini karibu Mashahidi 200 wameachwa bila makao. Maji yalifurika kufikia mita mbili katika Jumba la Ufalme, au nyumba ya ibada, lililoko katika eneo la Kaduwela, kilomita 15 kutoka Colombo.

Kikundi cha wajitoleaji katika Jumba la Ufalme la Kotahena wakitayarisha maji ya chupa, chakula, mavazi, na dawa kwa ajili ya walioathiriwa.

Upesi Mashahidi waliunda halmashauri ya kutoa msaada ili kusimamia kazi ya kushughulikia mahitaji ya kimwili ya walioathiriwa na pia wakawasaidia kiroho. Jumba la Ufalme la Kotahena lilitumiwa kuhifadhi vitu kama vile maji ya chupa, mavazi, na dawa. Mamia ya Mashahidi wa Sri Lanka walijitolea kuwagawia Mashahidi wenzao na majirani vitu walivyohitaji.

Nidhu David, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Sri Lanka, anasema hivi: “Tunaendelea kusali kwa ajili ya familia nyingi ambazo zimeathiriwa na msiba huu. Pia, tunawasaidia kusafisha nyumba zilizokumbwa na mafuriko, kugawa chakula, na kuwapatia nguo wote walioathiriwa. Roho ya kujitolea ambayo washiriki wetu wameonyesha imesaidia sana kuwatia watu moyo katika kipindi hiki cha matatizo.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi Habari za Umma, 1-718-560-5000

Sri Lanka: Nidhu David, 94-11-2930-444