Hamia kwenye habari

Kesi ilisikilizwa katika chumba hiki cha Mahakama Kuu Zaidi ya Usimamizi nchini Sweden

DESEMBA 18, 2019
SWEDEN

Sweden Imekubali Kwamba Mashahidi wa Yehova Ni Shirika la Kidini Linalochangia Ubora wa Jamii

Sweden Imekubali Kwamba Mashahidi wa Yehova Ni Shirika la Kidini Linalochangia Ubora wa Jamii

Tangu Januari 1, 2000, serikali ya Sweden imekuwa ikiyapa mashirika ya kidini msaada wa kifedha chini ya mpango wa Msaada kwa Mashirika ya Kidini. Msaada wa kifedha hutolewa kwa vikundi “vinavyodumisha na kuimarisha viwango vya kimsingi katika jamii” na “vilivyo imara na vinavyojihusisha na shughuli za kijamii.

Licha ya kwamba serikali ya Sweden iliamua kutoa msaada wa kifedha kwa dini nyingi kuanzia 2007, serikali hiyo ilikataa kuwapa Mashahidi wa Yehova msaada wa kifedha, kwa sababu ya msimamo wetu wa kutojihusisha na siasa.

Kwa kuwa hawakuwa na njia nyingine, ndugu zetu waliamua kuwasilisha mahakamani mashtaka dhidi ya serikali ya Sweden katika pindi tatu tofauti. Na kila mara, Mahakama Kuu Zaidi ya Usimamizi ilifikia mkataa kwamba uamuzi wa serikali wa kunyima shirika letu msaada wa kifedha ni kinyume cha sheria na kwamba uamuzi huo unapaswa kufikiriwa upya.

Hatimaye, Oktoba 24, 2019, serikali ya Sweden ilibadili msimamo wake na kuamua kwamba Mashahidi wa Yehova wanatimiza “matakwa yote ya kisheria” ya kupokea msaada wa kifedha kutoka serikalini.

Hivi karibuni, suala kama hili pia lilizushwa nchini Norway, kwa kawaida nchi hiyo hutegemeza mashirika yote ya kidini kifedha kutia ndani Mashahidi wa Yehova. Hata hivyo, miezi kadhaa iliyopita serikali iliombwa ichunguze tena msingi wa kuwapa Mashahidi wa Yehova msaada wa kifedha kwa sababu ya msimamo wao wa kutojihusisha na siasa. Hivyo, ndugu zetu waliwasilisha kwa wenye mamlaka huko Norway habari sahihi kuhusu msimamo wetu wa kutojihusisha na siasa. Hata waliwasilisha nakala ya hukumu ya Mahakama Kuu Zaidi ya Usimamizi nchini Sweden, pamoja na nakala nyingine za hukumu za mahakama na mabaraza ya usimamizi nchini Ujerumani na Italia.

Tunafurahi kwamba Novemba 18, 2019, wenye mamlaka nchini Norway waliamua kwamba Mashahidi wa Yehova wanapaswa kupokea msaada wa kifedha kutoka serikalini na kwamba: “Kupiga kura ni haki ya msingi ya raia wa Norway, lakini si jambo la lazima. Inaonekana kwamba kutotumia haki hiyo ni mojawapo kati itakadi za Mashahidi wa Yehova, . . . [lakini serikali] haioni kwamba jambo hilo . . . linaandaa msingi thabiti wa kisheria wa kuwanyima msaada wa kifedha.”

Ndugu Dag-Erik Kristoffersen, anayetumikia katika ofisi ya tawi ya Skandinavia, amesema hivi kuhusu uamuzi huo: “Tunafurahi kwamba tunatambulika kuwa watu wenye uvutano mzuri katika jamii. Tunatumaini kwamba nchi nyingine zenye mpango kama huu zitazingatia uamuzi huo.” Zaidi ya yote, tunamshukuru Yehova, Mpaji-sheria Mkuu.—Isaya 33:22.