Hamia kwenye habari

FEBRUARI 3, 2022
TAJIKISTAN

Kamati ya Umoja wa Mataifa: Haki za Ndugu Tierri Amedzro Zimekiukwa Nchini Tajikistan

Kamati ya Umoja wa Mataifa: Haki za Ndugu Tierri Amedzro Zimekiukwa Nchini Tajikistan

Desemba 14, 2021, Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu ilifikia uamuzi kwamba Tajikistan ilikiuka haki za kibinadamu za Ndugu Tierri Amedzro kwa kumkamata na kumwondoa nchini kwa lazima kumrudisha Kazakhstan.

Kamati hiyo ilifikia mkataa kwamba alikamatwa “bila sababu” na jambo hilo linakiuka Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa. Pia, kamati hiyo ilisema kwamba serikali haiwezi kumzuia Tierri kurudi Tajikistan ikiwa angependa kufanya hivyo. Maofisa nchini Tajikistan sasa “wako chini ya wajibu wa kufanya yote iwezayo ili kuzuia ukiukaji kama huo wa haki usitokee tena.”

Oktoba 4, 2018, wenye mamlaka nchini Tajikistan walivamia nyumba ambamo Mashahidi wa Yehova walikuwa wakiendelea na mkutano. Wenye mamlaka walimkamata Tierri na kumhoji kwenye makao makuu ya Kamati ya Serikali ya Usalama wa Kitaifa ya Tajikistan. Oktoba 16, 2018, hakimu alimhukumu Tierri eti kwa sababu ya kuhamia nchi nyingine bila kibali. Tierri ni raia wa Urusi anayefanya kazi nchini Tajikistan.

Hakimu alimtoza Tierri faini na akaagizwa aondoshwe nchini na kupelekwa Kazkhstan.

Tierri anasema hivi: “Ninatumaini kwamba uamuzi wa kamati hiyo ya Umoja wa Mataifa itasaidia kuboresha uhuru wa kidini nchini Tajikistan, na kwamba ndugu zetu waweze kumwabudu kwa amani ya akili.”

Kwa sasa kuna ndugu mmoja aliyefungwa nchini Tajikistan kwa sababu ya imani yake.

Tuna uhakika kwamba Yehova atawapa amani ya kudumu ndugu zetu wanaovumilia majaribu.​—Isaya 26:3.