Hamia kwenye habari

Ndugu Rustamjon Norov (wa pili kutoka kushoto) pamoja na mama yake, Fariza; ndugu yake, Ravshan; na baba yake, Batyr, walipotembelea ofisi ya tawi ya Kyrgyzstan mwaka wa 2016

OKTOBA 27, 2020
TAJIKISTAN

Ndugu Rustamjon Norov Amewekwa Mahabusu; Anakabili Miaka Mitano Gerezani Nchini Tajikistan

Ndugu Rustamjon Norov Amewekwa Mahabusu; Anakabili Miaka Mitano Gerezani Nchini Tajikistan

Hukumu Inatarajiwa

Mahakama ya kijeshi itatangaza a uamuzi wake hivi karibuni katika kesi kumhusu Ndugu Rustamjon Norov ambaye ni kijana. Anaweza kufungwa gerezani kwa miaka miwili hadi mitano kwa kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Amekuwa gerezani tangu Oktoba 1, 2020.

Maelezo Mafupi Kumhusu

Rustamjon Norov

  • Tarehe ya Kuzaliwa: 1998 (Dushanbe)

  • Maisha Yake: Alikuwa akifanya kazi ya kurekebisha nyumba na fanicha ili kujitegemeza yeye na familia yake. Anapenda kucheza mpira wa mguu

  • Alibatizwa 2016 akiwa na umri wa miaka 17. Baada ya miaka miwili, alihama kutoka kutaniko la lugha ya Kirusi ambalo familia yake inashirikiana nalo ili aweze kuwasaidia watu wanaozungumza Kitajiki kujifunza Biblia

Historia ya Kesi

Mwaka 2016, Ndugu Rustamjon Norov alijitolea kwa hiari kutoa taarifa katika ofisi ya kuandikisha utumishi wa jeshi. Aliwaeleza kuhusu msimamo wake wa kutounga mkono upande wowote na akaomba apewe utumishi wa badala wa kiraia. Mwaka uliofuata alifanya vivyo hivyo. Kamanda msaidizi wa ofisi ya kuandikisha utumishi wa jeshi, alimheshimu Ndugu Norov na alivutiwa sana na maelezo yake. Kwa miaka mitatu mfululizo, Ndugu Norov hakulazimishwa kujiunga na jeshi.

Lakini Septemba 24, 2020, Ndugu Norov aliitwa katika ofisi ya wilaya ya kuwaandikisha watu kwa ajili ya utumishi wa jeshi. Maofisa walimuuliza maswali kwa saa tatu na kufikia uamuzi wa kwamba anastahili kujiunga na jeshi. Kisha maofisa hao wakajaribu kumlazimisha afanyiwe uchunguzi na daktari. Baba ya Ndugu Norov alikuwepo wakati wa tukio hilo na akawaomba waipeleke kesi ya mtoto wake kwenye ofisi ya mwendesha-mashtaka.

Ndugu Norov na baba yake walifika katika ofisi ya mwendesha-mashtaka Oktoba 1. Mwendesha-mashtaka aliagiza ofisa wa polisi wa wilaya hiyo awapeleke kwenye ofisi ya wilaya inayowaandikisha watu kwa ajili ya utumishi wa jeshi. Walipofika, baba ya Ndugu Norov hakuruhusiwa kuingia ndani. Ndugu Norov aliwekwa chini ya ulinzi kwa siku mbili. Hakuwa ameshtakiwa au kuhukumiwa kwa kosa lolote. Alipokuwa chini ya ulinzi, maofisa walimzuia kuonana na wakili wake.

Oktoba 3, Ndugu Norov alihamishiwa kilomita 300 hivi kutoka mji wa Dushanbe ambapo familia yao inaishi, na kupelekwa kwenye kambi ya jeshi iliyo katika jiji la Khujand. Kwa siku mbili mfululizo, alihamishwa kutoka kambi mbalimbali katika jiji la Khujand.

Oktoba 6, Ndugu Norov aliruhusiwa kuipigia simu familia yake na kuonana na wakili wake. Hata hivyo, mahakama ya jeshi ya Tajikistan iliamuru apelekwe mahabusu. Ataendelea kukaa mahabusu mwendesha-mashtaka anapoendelea kufanya upelelezi na hadi mahakama itakapotoa hukumu. Ndugu Norov anashtakiwa kwa kosa la kutoa taarifa za uwongo kuhusu afya yake ili asijiunge na jeshi.

Ijapokuwa amefungwa, Ndugu Norov bado ni mchangamfu na anaendelea kumtegemea Yehova kabisa. Anamshukuru Yehova kwa kumsaidia kusitawisha imani na ujasiri anaohitaji ili kukabiliana na jaribu hili. Pia, anashukuru sana kwamba alipata jaribu lisilotarajiwa mwaka wa 2013. Mwaka huo, maofisa walikuja shuleni na kumchukua kwa nguvu Ndugu Norov na ndugu yake mdogo, Ravshan, na kuwapeleka katika ofisi ya kujiandikisha jeshini ili kuwafanyia uchunguzi wa afya. Wakati huo, Rustamjon alikuwa na umri wa miaka 15 tu, hivyo asingeweza kujiunga na jeshi. Pia, wakati huo alikuwa mhubiri ambaye hajabatizwa. Baada ya tukio hilo, baba yao, Batyr, aliamua kuwa atatumia wakati katika ibada ya familia ili kuwasaidia vijana wake kuwa na uwezo wa kutetea msimamo wao wa Kikristo wa kutounga mkono upande wowote. Mara kwa mara, Batyr aliigiza kama ofisa wa kuandikisha watu jeshini na vijana wake walifanya mazoezi ya jinsi ya kutetea imani yao.

Rustamjon anasema hivi: “Kabla ya kuwa na mazoezi hayo katika ibada ya familia, nilifikiri kwamba nilikuwa na uwezo wa kutetea imani yangu. Hata hivyo, tulipokuwa tukifanya mazoezi hayo, nilishangaa jinsi nilivyokuwa na wasiwasi na woga. Hali hiyo ilinisaidia nitambue kwamba nilihitaji kusali na kujifunza zaidi kuhusu imani yangu na uamuzi wangu wa kutounga mkono upande wowote. Pole kwa pole hofu yangu iliisha. Mwanzoni mwa 2016, nilijiweka wakfu kwa Yehova na kubatizwa.”

Rustamjon ametiwa moyo pia kwa kushirikiana na ndugu wakomavu, wenye umri mkubwa waliowahi kufungwa gerezani kwa sababu ya imani yao. Anasema hivi: “Ninatambua kabisa matokeo ya msimamo wa kutounga mkono upande wowote. Ikiwa nitafungwa gerezani, nitakuwa na pendeleo la kutakasa jina la Yehova katika ‘eneo jipya.’”

Baba ya Rustamjon anasema: “Familia yetu inamshukuru Yehova kwa pendeleo la kufanya mapenzi yake na kutumiwa kama vifaa katika mikono yake yenye upendo. Kwa familia yetu ya kiroho, tungependa kusema kwamba, ‘tunahisi upendo, sala, na msaada wenu wa kihisia na kiroho.’ Hatuna hofu wala wasiwasi. Amani ya Mungu inalinda mioyo yetu kama Yehova anavyotuhakikishia katika Neno lake!”—Wafilipi 4:6, 7.

a Tarehe ya hukumu haitangazwi mapema kila mara