SEPTEMBA 17, 2013
TANZANIA
Mahakama Kuu ya Tanzania Yatetea Haki za Kibinadamu za Wanafunzi Ambao Ni Mashahidi
DAR ES SALAAM, Tanzania—Julai 12, 2013, Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, ambayo ndiyo mahakama kuu zaidi nchini Tanzania, ilitoa uamuzi usiopingwa kwamba shule katika mkoa wa Mbeya zilikiuka uhuru wa kidini wa wanafunzi 127 ambao ama walifukuzwa shule au walipewa adhabu kwa kukataa kuimba wimbo wa taifa kwa sababu ya dhamiri.
Mnamo 2007, Kamati ya Shule ya Shikula iliwafukuza vijana watano Mashahidi kwa sababu walikataa kuimba wimbo wa taifa. Zaidi ya hilo, shule za msingi na za sekondari katika eneo hilo ziliwaadhibu vijana wengine 122 ambao ni Mashahidi kwa sababu hiyohiyo. Baada ya maombi yao kukataliwa na maofisa wa elimu na waziri mkuu, wanafunzi hao 127 walitafuta utatuzi wa kisheria katika Mahakama Kuu ya Tanzania, ambayo ndiyo mahakama ya pili kuu nchini humo. Mahakama Kuu iliunga mkono kwamba walipaswa kufukuzwa shuleni, ingawa uamuzi wa mahakama hiyo haukuungwa mkono na mahakimu wote. Kwa sababu hiyo, Desemba 2, 2010, wanafunzi hao walikata rufani kwenye Mahakama ya Rufaa. Kulingana na maandishi ya mahakama hiyo, uamuzi wa Mahakama ya Rufaa “unafutilia mbali” uamuzi wa Mahakama Kuu pamoja na kila kitu kilichohusika katika uamuzi huo.
Zadok Mwaipwisi, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Tanzania, anasema: “Tunafurahia uamuzi wa mahakama hiyo na pia tunafurahi kwamba umeunga mkono msimamo wa vijana hao unaotegemea dhamiri. Jambo hilo linategemeza haki ya kikatiba ya kwamba kila mtu ana uhuru wa ibada, si Mashahidi wa Yehova peke yake bali pia raia wote wa Tanzania.”
Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:
J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000
Tanzania: Zadok Mwaipwisi, simu +255 22 2650592