Hamia kwenye habari

DESEMBA 31, 2021
THAILAND

Gazeti Mnara wa Mlinzi Limechapishwa kwa Miaka Sabini na Tano Katika Lugha ya Thailand

“Muwe na Imani Katika Yehova, Mfanye Kazi kwa Bidii, na Mtapata Mtafsiri”

Gazeti Mnara wa Mlinzi Limechapishwa kwa Miaka Sabini na Tano Katika Lugha ya Thailand

Januari 1, 2022, itakuwa miaka 75 tangu toleo la kwanza la Mnara wa Mlinzi kutolewa katika lugha ya Thailand.

Habari njema zilihubiriwa kwa mara ya kwanza nchini Thailand mwaka wa 1931. Walipoanza kuhubiri, akina ndugu waliwapa watu, maelfu ya machapisho katika Kichina, Kiingereza, na Kijapani. Wakati huo, kijitabu kilichoitwa Protection ndicho tu kilichokuwa kimetafsiriwa katika Kithai.

Ndugu watatu, mapainia kutoka nchi nyingine, waliotumikia nchini Thailand, walitambua kwamba ili kugusa mioyo ya watu, walihitaji machapisho zaidi katika lugha ya Thailand. Ndugu Willi Unglaube alimwandikia barua Ndugu Rutherford na kuomba msaada. Ndugu Rutherford akamjibu: “Muwe na imani katika Yehova, mfanye kazi kwa bidii, na mtapata mtafsiri.”

Desemba 1939, Ndugu Kurt Gruber na Ndugu Willi Unglaube walikuwa wakihubiri kaskazini mwa Thailand. Chomchai Inthaphan, aliyekuwa mwalimu mkuu wa Shule ya Wasichana ya Kiprotestanti ya Chiang Mai, alipata chapisho la Kiingereza ambalo akina ndugu walikuwa wamegawa. Chomchai, ambaye alijua vizuri Kiingereza na lugha ya Thailand, alitambua kwamba alikuwa amepata ukweli.

Chomchai Inthaphan

Licha ya kupingwa na hata kuongezewa mshahara shuleni, baada ya muda mfupi Chomchai alijiuzulu shuleni na kanisani pia, na akabatizwa na kuwa Shahidi wa Yehova. Kitabu cha kwanza alichoombwa kutafsiri kilikuwa Salvation. Baadaye, Chomchai akawa mshiriki wa familia ya Betheli ya Bangkok na kwa miaka mingi alitumikia akiwa mtafsiri pekee wa lugha ya Thailand. Baada ya muda, wanawake kadhaa wenyeji walikubali kweli na wakastahili kusaidia katika kazi ya utafsiri.

Vita vya Pili vya Ulimwengu vilipoanza, utafsiri katika lugha ya Thailand ulisimama kwa muda, kisha ukaanzishwa tena, mara tu vita vilipokwisha. Toleo la Mnara wa Mlinzi la Januari 1947 lilitafsiriwa katika lugha ya Thailand, na nakala 200 zikachapishwa kwa mashine ya kunakili iliyokuwa katika makao ya wamishonari. Magazeti yaliendelea kuchapishwa kwa njia hiyo hadi 1952, ambapo magazeti 500 yalinakiliwa kila mwezi. Kisha akina ndugu wakaanza kuchapisha magazeti katika kiwanda cha kibiashara. Mnamo Septemba 1993 ofisi ya tawi ya Japani ilianza kuchapisha Mnara wa Mlinzi na Amkeni! katika lugha ya Thailand kwa ajili ya matumizi ya ulimwenguni pote.

Watafsiri wa lugha ya Thailand na Lugha ya Ishara ya Thailand, pamoja na vikundi vya kutokeza machapisho

Leo, ndugu na dada 80 hivi, baadhi yao wakiwa katika ofisi ya tawi ya Thailand na wengine katika ofisi mbili za utafsiri, wanasaidia katika kazi ya kutafsiri. Vilevile Mnara wa Mlinzi linatafsiriwa katika lugha ya Kiakha, Kilahu, Kilaotia, na Lugha ya Ishara ya Thailand.

Zaidi ya wahubiri 5,000 walio katika eneo linalosimamiwa na ofisi ya tawi ya Thailand, wanamshukuru Yehova kwa sababu gazeti Mnara wa Mlinzi linatafsiriwa katika lugha yao.​—Methali 10:22.