Hamia kwenye habari

Wajitoleaji wa ujenzi kwenye ukarabati wa ofisi ya tawi ya Thailand. Picha ndogo juu: Waliojitolea katika ujenzi sasa wanatumikia katika ofisi ya tawi ya Thailand. Picha ndogo chini: Mjitoleaji wa ujenzi (katikati) akihudhuria Shule ya Waeneza-Injili wa Ufalme

JUNI 28, 2023
THAILAND

Kusitishwa kwa Ujenzi wa Ofisi ya Tawi ya Thailand Kwatokeza Baraka Zisizotarajiwa

Kusitishwa kwa Ujenzi wa Ofisi ya Tawi ya Thailand Kwatokeza Baraka Zisizotarajiwa

Mradi wa ujenzi na ukarabati wa ofisi ya tawi ya Thailand ulianza katika mwaka wa 2019 kwa kutumia wajitoleaji nchini humo na wajitoleaji wa kimataifa. Hata hivyo, janga la COVID-19 lilipotokea, ni wafanyakazi 8 tu wa kimataifa kati ya 50 waliopewa mgawo kwenye mradi huo waliobaki. Wengine wote walilazimika kurudi kwenye nchi za nyumbani kwao. Kazi ilianza tena kadiri vizuizi vya janga hilo vilivyoendelea kuondolewa. Wajitoleaji wengi zaidi nchini humo walialikwa ili kupata mazoezi na kusaidia kukamilisha mradi huo. Sehemu ya mwisho ya kazi hiyo ilikamilishwa Aprili 30, 2023.

Ndugu Setthasat Tawansirikul na mke wake, Waraporn, walikuwa miongoni mwa wajitoleaji hao wa Thailand. Mwanzoni waliogopa kwa sababu hakuwa na uzoefu wa kazi. Ndugu Setthasat anasema hivi: “Tulipofika huko, tulifundishwa kwa njia yenye kustaajabisha.”

Shangwe na uradhi ambao wajitoleaji nchini humo walipata kwa kushiriki mradi huo uliwachochea wengi kati yao kujitoa katika nyanja nyingine za utumishi wa wakati wote. Baadhi yao sasa wanafanya kazi katika miradi ya ujenzi katika eneo lote la ofisi ya tawi ya Thailand. Dada mmoja anahudhuria Shule ya Waeneza-Injili wa Ufalme. Wengine sasa wanatumikia Betheli. Mmoja kati ya washiriki hao wapya wa familia ya Betheli, Ndugu Rapeepat Woradetsakul, anasema hivi: “Kujionea msaada wa Yehova wakati wa mradi huo wa ujenzi kulinipa uhakika niliohitaji kukubali mwaliko wa kutumikia Betheli. Nina uhakika kwamba Yehova atanisaidia katika mgawo huu mpya.”

Picha iliyopigwa kutoka juu ya majengo ya ofisi ya tawi ya Thailand yaliyofanyiwa ukarabati. Picha ndogo juu: Ndani ya ofisi zilizofanyiwa ukarabati. Picha ndogo katikati: Jengo jipya la udumishaji na kuhifadhi vitu. Picha ndogo chini: Eneo jipya la kuegesha magari

Kazi ya ujenzi na ukarabati kwenye ofisi ya tawi ya Thailand ilitia ndani kukarabati vyumba vya kulala na maeneo ya ofisi, kujenga jengo jipya la udumishaji na la kuhifadhi vitu, na kujenga eneo jipya la kuegesha magari. Mbali na hilo, nyumba sita zilizo karibu na ofisi ya tawi zilinunuliwa na kufanyiwa ukarabati ili kuandaa makao ya ziada kwa ajili ya washiriki wa familia ya Betheli.

Tunashangilia kwamba ndugu na dada zetu nchini Thailand wamejitoa kwa hiari katika utumishi wa Yehova na wanajionea ukweli wa maneno ya Zaburi 34:8: “Onjeni mwone kwamba Yehova ni mwema.”